NA MWANDISHI WETU
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi Bwawa la Kidunda litakalojengwa mkoani Morogoro na kugharimu sh bilioni 335.
Bwawa hilo litakua na uwezo wa kuhifadhi maji kwa miaka mitatu mfululizo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Morogoro, Kaimu Afisa Mtendaji DAWASA, Kiula Kingu amesema lengo la utekelezaji mradi huo ni kuwezesha mitambo ya maji ya Ruvu juu na Ruvu chini kuwa na maji ya kutosha ili kuzalisha maji kipindi cha kiangazi.
Aidha, Kingu amebainisha kuwa bwawa hilo litakapokamilika litakuwa lina hifadhi maji kipindi cha masika ili maji hayo yaweze kutumika nyakati za kiangazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Morogoro Mjini ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya, Rebeca Msemwa ameipongeza Serikali kwa udhubutu wa utekelezaji wa mradi na kutoa wito kwa DAWASA kuusimamia na kuutekeleza mradi kwa ukamilifu ili ulete manufaa kwa Watanzania.
Mbali na upatikanaji wa maji kwa uhakika, Kiula ameeleza faida za mradi huo na namna utakavyotoa fursa mbalimbali kwa Taifa ikiwemo ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 101, uzalishaji wa umeme megawatt 20, uvuvi na utalii ambavyo kwa pamoja vitawanufaisha wananchi kwa maeneo husika kwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Tunajivunia utekelezaji wa mradi huu katika Mkoa wetu wa Morogoro, Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha kiangazi hivyo hatuna budi kuunga juhudi hizi kwa kuhakikisha DAWASA wanatekeleza mradi huu kwa ukamilifu kama ilivyo matarajio ya Watanzania “. Alisisitiza
Naye, Mkurugenzi wa Bonde la Wami Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi ameeleza mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha vyanzo vyote vinavyoingia katika bwawa la Kidunda linakuwa na maji ya kutosha kwa kuzuia shughuli zote za uharibifu zinazosababishwa na binadamu au mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Tumejipanga kufanya uthamini na tathmini katika maeneo yote yanayozunguka chanzo cha mto Ruvu na kutangazwa kuwa maeneo ya uhifadhi kwa kutenga shilingi bilioni nne ili kuhakikisha bwawa la Kidunda linatoa suluhu ya upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani”. amesema Mmasi