NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ndio Mratibu wa ushirikiano na uhusiano baina ya Tanzania na nchi nyingine duniani katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii imesema kuwa, ziara za viongozi wetu wa kitaifa nje ya nchi zimeliletea taifa mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Stergomena Tax ameyasema hayo leo Mei 30, 2023 jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Kwa ujumla ziara hizi za Rais wa Awamu ya Sita, Dk Samia Suluhu Hassan na Viongozi wengine Wakuu zimeimarisha uhusiano wa Kimataifa baina ya nchi yetu na nchi rafiki, Jumuiya za Kikanda, na Jumuiya za Kimataifa na kuleta mafanikio makubwa kiuchumi na kijamii ikiwemo ongezeko la uwekezaji, kufungua masoko ya bidhaa mbalimbali, ongezeko la watalii, upatikanaji wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa miradi mbalimbali katika sekta za kijamii na kiuchumi “, amefafanua Dk Stergomena.
Ametaja mafanikio ya ziara hizo kuwa ni; heikh Tamim Bin Hamad Al Thani, Amiri na Mtawala wa Dola ya Qatar kuahidi kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa masomo ya afya, kujenga jengo la mama na mtoto na kuleta wataalamu wa afya nchini kwa lengo la kubadilishana ujuzi, ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari na kusaidia baadhi ya miradi ya kimkakati ya maendeleo ya Tanzania kupitia mfuko wa Maendeleo wa Qatar, Tanzania na Oman kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano katika sekta za elimu ya juu na mafunzo ya ufundi, utunzaji wa nyaraka na ujenzi wa kituo cha uhifadhi wa taarifa.
Mafanikio mengine ni Tanzania na China kusaini Hati ya Makubaliano kuruhusu zao la parachichi kuingia katika soko la China na Hati ya Makubaliano kuruhusu mazao ya uvuvi yakiwemo mabondo ya samaki kutoka Tanzania kuingia katika soko la China, Serikali ya Watu wa China kuipatia Tanzania mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 297.64 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa mawasiliano vijijini, msaada wa Dola za Marekani milioni 24.86 kwa ajili ya upanuzi wa JKCI na mkopo wa Dola za Marekani milioni 58.3 kwa ajili ya kugharamia upanuzi wa Jengo la 3 la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume Zanzibar.
Vilevile, Serikali ya China kutekeleza mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa 400 KVA North East Transmission Line na kuendelea kutoa msaada wa ujenzi wa vyuo vya ufundi (VETA) nchini Tanzania, kutengwa kwa Dola za Marekani milioni 550 ili kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika na kuandaa Mpango wa Miaka Mitano (2023 – 2027) na kuridhiwa kwa ombi la Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Mapinduzi ya Kilimo Afrika (AGRF) unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba 2023 na Serikali ya Jamhuri ya Korea imeahidi kushirikiana na Tanzania kujenga Chuo cha Teknolojia ya Kidijitali ambacho kitakuwa cha kipekee Afrika Mashariki na Kati.
Pia, Serikali ya Jamhuri ya Korea itaipatia Tanzania mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 70 kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mfumo wa vitambulisho vya Taifa, Dola za Marekani milioni 65 kwa ajili ya mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya upimaji na ramani na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano kati ya kampuni za uzalishaji dawa na vifaa tiba za Korea na Bohari ya Dawa Tanzania kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kunufaika na ufadhili wa Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza miradi ya nishati jadidifu kupitia Mfuko wa Teknolojia ya Nishati Salama uliotengewa Dola za Marekani bilioni 1.2 na Benki hiyo.