NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Miundombinu na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa amewasilisha mpango wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Ameliomba Bunge kuidhinisha takribani kiasi cha Sh trilioni 3.6 ili kuiwezesha Wizara kuifungua nchi kupitia barabara.
Katika hotuba yake aliyoiwasilisha Dodoma leo Jumatatu, Mei 22, 2023, Prof Mbarawa ameliaambia Bunge kuwa mbali na mambo mengine yatakayotekelezwa 2023/24, barabara saba zenye jumla ya urefu wa kilometa 2,035 zitaanza kujengwa kwa kiwango cha kupitia utaratibu wa EPC + F.
Ameainisha barabara hizo kuwa ni Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha/Songea (km 435), Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (Simiyu) (km 339) na ile ya Handeni – Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboroti – Mrijochini – Dalai – Chambalo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (km 460).
Nyingine ni barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa Junction (km 453.42), Masasi – Nachingwea – Liwale (km 175), Igawa – Songwe – Tunduma (km 218) pamoja na barabara ya mchepuo ya Uyole – Songwe yenye urefu wa kilometa 48.9 pamoja na Mafinga – Mtwango – Mgololo (km 81).
Amesema miradi hiyo na mingine ya kimkakati itaweza kutekelezwa ikiwa kiasi kilichoombwa kitaidhinishwa.
Akitoa mchanganuo wa fedha hizo, Prof Mbarawa amesema kati ya fedha hizo, Sh trilioni 1.5 ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi na Sh trilioni 2.09 ni kwa ajili ya sekta ya Uchukuzi.