NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SERIKALI imepokea kiasi cha Sh.Bilioni 6 kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni sehemu ya gawio la kiasi cha Sh. Bilioni 20 ambayo benki hiyo imetenga kwa ajili ya wanahisa wake kufuatia faida iliyopata katika kipindi cha mwaka 2022. Serikali inamiliki asilimia 30 ya hisa za benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi alikabidhi gawio hilo kwa Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu aliyewakilisha serikali wakati hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika mapema leo Mei 17, 2023 jijini Dar es Salaam ikihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka serikali na maofisa waandamizi wa benki hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mchechu pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2022, aliwasilisha salamu za Rais Dk Samia Suluhu ambae pia aliipongeza benki hiyo huku akitoa wito kwa taasisi na mashirika yenye umiliki wa umma kuhakikisha yanatimiza wajibu wao wa kuwasilisha gawio limetokana na faida za uendeshaji wa shughuli zao kwa serikali.
“Serikali inafurahishwa na utendaji ulioimarika wa Benki ya NBC. Sisi kama wanahisa, tunafurahi kuona uwekezaji wetu unatoa matunda. Gawio la Sh.Bilioni 6 ambalo Serikali ilipokea leo litaongeza ukubwa wa kapu letu la makusanyo ambayo yamekuwa yakielekezwa katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ile ya kimkakati. Hivyo Naipongeza sana Benki ya NBC kwa mafanikio haya…hongereni sana,’’ amesema Mchechu.
Aidha Mchechu alitumia fursa hiyo kuwasilisha agizo la Rais Samia Suluhu unaoyaka mashirika na taasisi nyingine zenye umiliki wa umma kuhakikisha zinatimiza wajibu wao wa msingi wa kuwasilisha gawio kwa serikali.
“Anachosisitiza Mheshimiwa Rais kwenye hili ni kwa taasisi hizi kutimiza wajibu huu kwa fedha zitokanazo na faida iliyopatikana tu na si kwa taasisi hizi kukopa mahali popote ili kulipa gawiwo. Hata hivyo taasisi zitakazoshindwa kutimiza wajibu ipo haja ya viongozi wa taasisi hizi kujitafakari ili kuona kama kweli wanastahili kuendelea kuongoza taasisi zisizo tengeneza faida kwa taifa,’’ amesema.
Awali akizungumza kwenye tukio hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, alieleza kuwa mafanikio na mwenendo chanya wa benki hiyo unathibitisha imani kubwa waliyonayo wateja kwa kwa Benki hiyo.
“Tuna furaha kusalia katika dhamira yetu ya kufikia malengo yetu muhimu katika kupanua nyayo zetu na kuwekeza katika teknolojia ili kuboresha uzoefu wa wateja wetu. Faida yetu ya kabla ya kodi ilikua kwa asilimia 36 hadi Sh.Bilioni 81.9 kutoka Sh.Bilioni 60 Desemba 2021.’’
“Ongezeko hili la faida ndilo linatuwezesha kutoa Sh.Bilioni 20 kama gawio kwa wanahisa wetu; leo, tunafurahi kukabidhi hundi ya Sh.Bilioni 6 kama gawiwo kwa mwaka 2022. Tunatazamia mustakabali wenye matumaini zaidi huku pia tukiwa tunaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu.” amesema Dk Doriye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa taasisi za fedha kama Benki ya NBC kustawi huku pia akiipongeza Bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo pamoja na wafanyakazi kwa jitihada kubwa walioifanya hadi kufikia mafanikio hayo.
“Utendaji kazi wa Benki unaonyesha mazingira bora ya biashara ambayo yalituruhusu kuwafikia wateja wetu kwa urahisi. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua nyayo zetu na kuboresha huduma zetu zetu ili kukidhi na kuzidi matarajio ya wateja wetu.” amesema Sabi.
Akizungumzia uwajibikaji wa benki hiyo kwa jamii Sabi amesema katika kipindi cha mwaka 2022 benki hiyo ilifanikiwa kukusanya pesa kiasi cha Sh.Milioni 200 kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon 2022 ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
“Benki ya NBC ndiyo mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania ‘NBC Premier League”, ambayo inazalisha ajira na kusaidia uwezeshaji na ushirikishwaji wa kifedha.’’ ameliongeza Sabi huku akibainsha kuwa benki hiyo iliongeza matawi matano mapya katika kipindi cha mwaka wa 2022 huku wakala wa mtandao wa benki hiyo “NBC Wakala” ukikuwa kwa asilimia 82 kutoka mawakala 5,121 hadi 9,525.
