NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
WAKAZI wa 4200 wa Vikuruti Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wanatarajia kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya baada ya ujenzi wa Zahanati iliyojengwa kwa fedha za Halmashauri na wananchi zipatazo Mil.152/-
Hayo yamebainishwa na Mganga mkuu wa Halmashauri Wilaya hiyo Wilford Kondo alipokuwa akitoa taarifa wakati Mwenge wa Uhuru ulipopita kukagua na kuweka jiwe la msingi katika zahanati hiyo.
Dk.Kondo amesema awali wananchi hao walikuwa wakitembea km sita kufuata huduma za afya na kwamba kwasasa ujenzi wa Zahanati hiyo umefikia asilimia 85 .
Amesema lengo la mradi huo ni kusogeza huduma karibu na wananchi ambapo kaya 840 katika Kitongoji cha Vikuruti na vingine vya jirani vitanufaika na zahati hiyo.
Dk Kondo amebainisha kuwa kati ya fedha hizo Sh. Milioni 150 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na Sh. Mil. 2.5 zilitokana na nguvu za wananchi.
Awali akitoa taarifa baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Bagamoyo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon amesema Mwenge huo utakimbizwa katika miradi 14 ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha yenye thamani ya Sh. Trillioni 3.1