NA BENNY MWAIPAJA, DAR ES SALAAM
TANZANIA na Japan kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA), zimesaini mikataba mitatu ya mkopo wenye masharti nafuu na msaada, yenye thamani ya Yen bilioni 10.15, sawa na shilingi za Tanzania, bilioni 174.9, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Ununuzi wa pemebejeo za kilimo pamoja na kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).
Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo kwa niaba ya Serikali, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk.Natu Mwamba, alisema kuwa Yen bilioni 10 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 172.2 ni mkopo nafuu uliotolewa na Shirika la Ushirikiano la Kimataifa (JICA) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kiasi cha Yen milioni 150, sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 2.6, ni msaada uliotolewa na nchi hiyo kupitia Ubalozi wake hapa nchini.
Dk.Mwamba, alisema kuwa mkopo huo utatumika kuongeza tija katika kilimo kwa kununua pembejeo ikiwemo mbolea, mbegu bora kwa ajili ya wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kipaumbele ambayo ni mpunga, ngano na alizeti na kuweka mifumo bora ya upatikanaji wa chakula na lishe.
Aliitaja mikoa itakayonufaika na mradi huo wa kuendeleza kilimo kuwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Morogoro, Tabora, Songwe, Mbeya, Njombe, Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu na Katavi.
Kuhusu mradi wa kuendeleza sekta ya Uvuvi, Dk.Mwamba alisema kuwa shilingi bilioni 2.6 zilizotolewa na Japan kama msaada, zitatumika kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), ikiwa ni nyongeza ya fedha za msaada wa Yeni milioni 200 sawa na shilingi bilioni 3.5 zilizotolewa na nchi hiyo kupitia mkataba uliosainiwa mwezi Disemba mwaka 2019 na hivyo kuufaya kufikia shilingi bilioni 6.2, lakini utekelezaji wake ulikwama baada ya kuzuka kwa UVIKO 19.
Kwa upande wao, Balozi wa Japan Nchini Tanzania, Yashushi Misawa na Mwakilishi Mkazi wa (JICA), Hitoshi Ara, walisema kuwa mkopo na msaada huo umelenga kukabiliana na uhaba wa chakula unaoikabili dunia hivi sasa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uharibifu wa mazingira, vita vya Urusi na Ukraine pamoja na UVIKO 19.
Walisema kuwa Vitu hivyo vimeleta changamoto kubwa kwa sekta ya kilimo na usalama wa chakula kwa jumuiya ya kimataifa huku Afrika ikitajwa kuwa bara lililoathiriwa zaidi, na kuupongeza uongozi madhubuti wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa chakula na kufikia malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula barani Afrika” Alisema Balozi Misawa
“Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania kupitia JICA kwa zaidi ya miaka 60, ikihusisha maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maendeleo ya kilimo na uvuvi. Na kila mara tunajikumbusha kuwa maendeleo ya rasilimali watu yanapaswa kuwa nguzo muhimu katika aina yoyote ya usaidizi wa maendeleo” Alisema Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yashushi Misawa
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, alisema kuwa fedha za msaada kutoka Japan, zitatumika kununua meli kubwa ya uvuvi katika Bahari Kuu ya Hindi, kujenga miundombinu ya kuhifadhi samaki pamoja na vitendea kazi vingine vitakavyo tumika kuinua sekta ya uvuvi na kuiingizia Serikali fedha za kigeni.
Alisema kuwa mradi huo ambao utatekelezwa kwa kipndi cha mwaka mmoja utakapo kamilika, pamoja na mambo mengine, unatarajia kuongeza ajira 20,000, na kuiingizia Serikali zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka hivyo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mchango wa sasa wa asilimia 1.7.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dkt Hussein Omar aliishukuru Japan kupitia JICA kwa kuwekeza kiasi hicho cha fedha katika sekta ya kilimo ambayo imeajiri idadi kubwa ya watu.
Alisema kuwa fedha hizo zitasaidia kuboresha kilimo kwa kuwawekea wakulima mazingira bora ya uzalishaji ikiwemo kuwapatia wakulima wadogo mbolea, mbegu bora, viuatilifu na huduma nyingine za ugani ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi.