NA MWANDISHI WETU, TANGA
MKUU wa mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amewataka viongozi katika mkoa huo wakiwemo wakuu wa wilaya kila mmoja katika wilaya yake kutowaonea haya wanaoharibu mazingira na badala yake kuwachukulia hatua kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho.
Kindamba ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti mkoa wa Tanga mwaka 2023 iliyofanyika Aprili 27, 2023 yenye lengo la kutoa hamasa kwa wananchi kila mmoja kuweza kuhamasika kupanda miti katika maeneo yao.
” Nawaomba wakuu wa wilaya mkalisimamie hilo hawawezi watu wakawa wanakata miti halafu tunacheka nao ukicheka na nyani utavuna mabua na sisi Mkoa wa Tanga hatutotaka kuvua mabua” amesema Kindamba
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema maelekezo ya viongozi akiwemo Rais Dk. Samia yapo wazi katika kutunza mazingira sambamba na vyanzo vya maji hivyo maelekezo hayo yasimamiwe kwa ukamilifu na kwa wakati .
Pia Kindamba ameeleza kuwa kampeni hiyo ikitiliwa mkazo itaenda kuleta manufaa makubwa katika kulinda mazingira.
“Ndugu zangu tunakampeni ya kupanda miti isiyopungua milioni moja laki tano kila mwaka ni kampeni ambayo tukiweza kukomaa vizuri tukapambana vizuri tunaiweza” amesema Kindamba
Kwa upande wake katibu Tawala Mkoa wa Tanga , Pili Mnyema amewataka viongozi wote katika mkoa huo kusimamia vyema kampeni hiyo ya upandaji miti kuhakikisha inafanikiwa kwa asilimia mia moja.
Kampeni ya upandaji miti mkoa wa Tanga mwaka 2023 imebebwa na kauli mbiu isemayo ” mazingira yangu, nchi yangu naipenda daima”