MOJA ya kampuni kubwa ya mitandao ya kijamii, Twitter imeanza kurejesha ‘bluetick’ kwa wateja wasiolipia huduma hiyo.
Kampuni hiyo yenye makao makuu nchini Marekani inayomilikiwa na tajiri namba moja duniani, Elon Musk ambayo ina watumiaji zaidi ya milioni 450 kwa mwezi, imeanza zoezi za kuwarejeseha bluetick wateja wenye wafuasi zaidi ya milioni moja.
Mapema Machi ikiwa ni wiki chache tu kabla ya Elon Musk kukamilisha ununuzi wa mtandao huo, lilitoka tangazo kuwa wale wote wanaotaka kuwa na bluetick wanapaswa kulipia Dola za Marekani 8 kila mwezi (Tsh. 16,000) ili kupata huduma hiyo.
Watumiaji wengi ambao hawakuwa na bluetick wakaanza kulipia na kupata bluetick ambapo awali ulikuwa unaomba na kupewa bure na kampuni hiyo kama wakijiridhisha kuwa mmiliki wa akaunti ni ni mtu anayeaminika kwenye jamii yake.
Baada ya tangazo hilo la kulipia huduma hiyo, likaja tangazo lingine lililotoa taarifa kuwa wale wote wenye bluetick wasipolipia ifikapo Aprili 20, wangeanza kuondolewa bluetick kwenye akaunti zao.
Ilipofika tarehe hiyo, wengi walianza kuondolewa akiwemo mwanamuziki maarufu nchini Tanzania, Nasib Abdul (Diamond Platnumz) na Nick Minaj wa Marekani.
Lakini kuanzia jana Jumamosi, Aprili 22, 2023 baadhi ya akaunti zilizoondolewa bluetick zilirejeshewa huduma hiyo bila kulipia.
Miongoni mwa watu maarufu wa Tanzania waliorejeshewa bluetick ni pamoja na Mwanahabari na Mwanaharakati Maria Sarungi mwenye wafuasi milioni 1.1 pamoja na Mwanasheria na Mwanaharakati Fatma Karume mwenye wafuasi milioni 1.
Maria na Fatma waliweka ujumbe kwenye akaunti zao wakishangaa kurejeshewa huduma hiyo leo bila kulipia.