NA JOSEPH MAHUMI, WFM, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Bima la China (CHINA EXPORT AND CREDIT INSURANCE CORPORATION (SINOSURE), limeahidi kuendelea kudumisha ushirikiano na Tanzania ambao umekuwepo kwa muda mrefu kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya watu.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Zha Weimin alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Mwigulu Nchemba (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.
Weimin amesema SINOSURE inafanya juhudi kuwezesha ushirikiano kati ya Tanzania na China kuwa wenye matokeo chanya kwa kushawishi kampuni nyingi za China kuwekeza katika miradi mbalimbali na kufanya biashara Tanzania.
“Wafanyabiashara wengi wa China wanawiwa kufanya biashara na Tanzania hivyo jitihada mbalimbali vinazofanyika katika kupunguza vikwazo vya kibiashara na kurekebisha sera katika ushirikiano wetu zitasaidia kuboresha zaidi uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili” amesema Weimin
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Nchemba, amewahikikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kujidhatiti kufanya kazi na kushirikiana na Serikali ya China ili kuboresha ushirikiano wa nchi hizo mbili ambao umekuwepo kwa muda mrefu ili kuleta maendeleo ya wananchi.
Dk.Nchemba alisema kuwa Tanzania inatekeleza ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Reli ya kisasa(SGR )ambao utaunganisha Tanzania na nchi jirani na ameliomba Shirika hilo kusaidia utekelezaji wa mradi huo Lot 5 kutoka Isaka hadi Mwanza (Km 341) na Lot 6 kutoka Tabora hadi Kigoma ambayo ni takriban Kilometa 506, zote zinatengenezwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Company (CRCC).
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa msaada mkubwa kwa sekta mbalimbali za uchumi wetu ikijumuisha Miundombinu ya Reli, Elimu, TEHAMA, Nishati, Maji, Usalama, Viwanda na Sekta za Afya. Ni matumaini yetu kuwa ushirikiano huu wa pamoja utaendelea kuimarika zaidi” amesema Dk. Nchemba.