NA MWANDISHI MAALUM, DAR ES SALAAM
KWA mara ya kwanza nchini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila iliyopo jijini Dar es Salaam, imefanya utoaji wa figo kupitia njia ya tundu dogo na kupandikiza figo kwa wagonjwa watatu kwa siku mbili.
Aina hiyo ya utoaji wa figo kutoka kwa mchangiaji hufanya kazi hiyo kuwa rahisi kutokana na kupona haraka, kutumia muda mfupi na kidonda kidogo.
Daktari bingwa wa upasuaji, mfumo wa mkojo na figo, Hamisi Isack amesema kwa aina hiyo ya upandikizaji figo wanafanya utoaji figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia tundu dogo, ambapo awali upasuaji wa kawaida wa kuchana na kutoa figo na kumpandikiza anayepokea ulifanyika.
“Lakini kwa njia ya hii ya matundu madogo inamrahisishia mchangiaji kuwa na maumivu kidogo na uponaji wake ni rahisi,” amesema na kuongeza:
“Inaokoa gharama ya kukaa hospitali siku mbili au tatu na baada ya muda mfupi anarudi katika hali yake tofauti na anayechanwa inatumia muda mrefu na maumivu pia.”
Dk Isack amesema mtu akiwa na figo moja anaishi kawaida kama wengine wala hatakuwa na shida tena.
Ameishukuru serikali kwa kuwezesha miundombinu na vifaa tiba ambayo imewezesha kukamilisha aina hiyo ya upasuaji, ambayo imefanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Mmoja wa wagonjwa waliopandikizwa figo, mkazi wa Mkoa wa Simiyu,Wilaya ya Bariadi, Mwaisumbe Joseph amesema alianza kuumwa figo 2016, lakini alianza kusafishwa damu mwaka 2020 huku changamoto kubwa ilikuwa kupata fedha na mtu wa kumtolea figo, lakini sasa anashukuru kaka yake kamtolea figo na anaendelea vizuri.
“Changamoto nyingine ni imani za kishirikina lakini pia nilitumia dawa za kienyeji na hazikunisaidia, nikaachana nazo nikawa nasafisha nashukuru sasa nimepandikizwa,” amesema.
Ameeleza kuwa wakati anaumwa alikuwa anashindwa kupumua vizuri, alikuwa anakosa mkojo lakini sasa anaendelea vizuri kwani ilikuwa gharama kubwa kupata fedha za kusafisha figo.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi Hospitali ya Mloganzila, Dk Julieth Magandi amesema, wiki mbili zilizopita Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Prof Mohammed Janabi alitangaza kuanzisha huduma mpya ya kibingwa sasa tukio hilo limeweza kutekelezeka.
“Hospitali mbili tu zinatoa huduma za upandikizaji figo, 2017 ilianza Muhimbili na baada ya muda Hospitali ya Benjamini Mkapa na Mloganzila imekuwa ya tatu sasa ni tukio la kihstoria,” amesema