NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan ameelekeza maadhimisho sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yafanyike katika ngazi ya mikoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi
Hayo yamesemwa kwa niaba ya Rais Dk Samia na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana Jumamosi Aprili 15, 2023 wakati alipozindua Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)-Tunguu.
Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dk Samia ameelekeza shughuli za maadhimisho hayo zifanyike kuanzia Aprili 17 , 2023 hadi siku ya kilele Aprili 26 , 2023.
Majaliwa amesema kuwa maadhimisho hayo ambayo yatafanyika kupitia Mikoa, Taasisi za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama yaambatane na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, shughuli za kijamii hususan upandaji miti, usafi wa mazingira na mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali.
Kadhalika, yaambatane na Mashindano ya uandishi wa Insha kwa shule za Msingi na Sekondari, mahojiano maalum na Wazee maarufu, midahalo na makongamano kuhusu Muungano na hatua ya maendeleo iliyofikiwa hadi sasa.
“Majengo yote ya Serikali yapambwe kwa vitambaa vyenye rangi sahihi za bendera ya Taifa, picha za Waasisi wa Muungano, Picha ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Tanzania Bara” amesema Waziri Mkuu
Amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar majengo yapambwe kwa rangi sahihi za bendera ya Taifa, na picha za Waasisi wa Muungano na picha ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka huu ni “UMOJA NA MSHIKAMANO NDIYO NGUZO YA KUKUZA UCHUMI WETU”.