NA DENIS SINKONDE, SONGWE
ZAIDI ya wanafunzi 60 wa kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari ya kutwa Vwawa iliyopo katika mji wa Vwawa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamenusurika kifo baada ya bweni lao kuteketea kwa moto asubuhi ya Aprili 14, 2023 wakiwa darasani na wengine kwenye mitihani ya kujipima kimkoa.
Kaimu Kamanda Jeshi la Zima moto na uokoaji mkoa wa Songwe Inspekta Eleutery Mremi akiongea na Vyombo vya Habari kwenye tukio hilo amesema wamepata wito wa tukio hilo la moto saa tatu asubuhi, ambapo walikuta moto umeunguza bweni zaidi ya asilimia 50.
Amesema wamechelewa kulifikishia taarifa jeshi la Zima moto hivyo kukuta mali nyingi za wanafunzi hasa, nguo , vitanda magodoro vimeteketea kwa moto huo ambao bado chanzo chake hakijajulikana.
“Tumekuta bweni limeteketea kwa zaidi ya asilimia 50, tulichofanya ni kuokoa mabweni mengine na madarasa yasipate moto na kuteketea, pia tumefanikiwa kudhibiti moto huo kwa asilimia 99” amesema Inspekta Mremi.
Amesema katika tukio hilo hakuna kifo wala majeruhi yeyote. na kudai kuwa uchunguzi unaendelea ili kugundua chanzo cha moto huo, huku tathmini ya mali zilizoteketea ikiendelea kufanyika
Ofisa elimu mkoa wa Songwe Michael Ligola amesema Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi baada ya tukio hilo wameungana kuwasaidia wanafunzi walioathirika na tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwanunulia magodoro na vifaa vya kujifunika.
Amesema wanaendelea kufanya tathmini ya mali zote zilizoteketea kwa moto , ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi kujua chanzo cha tukio hilo la moto ambalo ni mara ya kwanza kutokea katika shule hiyo.
” Tunashukuru pamoja na madhara makubwa ya kuteketea kwa mali mbalimbali za wanafunzi, hakuna mwanafunzi Hata mmoja aliye poteza maisha wala kupata majeraha, kwa sababu ulitokea wakiwa madarasani wakiendelea na masomo , huku wengine wakiendelea na mitihani ya kujipima ya mkoa” amesema Ligola.
Aidha Ligola amewataka wanafunzi ambao mabweni yao yapo salama kutoa ushirikiano kwa wenzao ambao ni waathirika wa tukio hilo.
Amesema kuwa wenzao wanahitaji misaada mbali mbali ya nguo, daftari za kusoma na vitabu wapewe ushirikiano wa kutosha.
Akielezwa juu ya tukio hilo, mwanafunzi Gospel Andwale kidato cha sita amesema walikuwa darasani wakapata taarifa ya ghafla kuwa bweni lao linaungua, walipojaribi kwenda kuokoa vifaa vyao walikuta tayari vimeungua.
“Tumebaki na nguo tulizokuwa tumevaa tukiwa darasani , kila kitu kimeungua madaftari, nguo, magodoro na vitabu .tunaomba viongozi wa shule, Wilaya na mkoa watusaidie Ili tuweze kupata baadhi ya mahitaji ambayo ni muhimu” amesema Gospel.