NA DENIS SINKONDE, SONGWE
BWENI la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Vwawa iliyopo Wilayani Mbozi mkoani Songwe limeteketea kwa moto.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa Eleutery Mremi amesema moto huo umeanza asubuhi ya Aprili 14, 2023 asubuhi.
Kamanda Mremi amesema bweni hilo lilikuwa linatumiwa na wanafunzi 64 ambapo vitu vilivyokuwemo ndani ya bweni hilo vimeteketea na wakati moto huo unatokea wanafunzi walikuwa darasani wakiendelea mitihani.
“Hakuna majeraha wala vifo vilivyosababishwa na moto huo huku tathimini ikiendelea ya malizi zilizoteketea”, amesema kamanda Mremi.
Kamanda Mremi amesema jeshi hilo limefanikiwa kuudhibiti moto huo usienee kwenye mabweni mengine na madarasa na hadi sasa chanzo cha moto kinachunguzwa.
Kamanda Mremi amesema moto huo umeenea kwenye mabweni hayo kutokana na kuchelewa Kwa taarifa lakini jitihada za haraka za jeshi la zimamoto zimeweza kuudhibiti moto huo.