NA MWANDISHI WETU, NJOMBE
JESHI la Polisi mkoani Njombe limemkamata mfanyabiashara mmoja(jina linahifadhiwa) kwa tuhuma za kuchoma maduka ya Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT -CCM) Wilaya ya Njombe.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Hamis Issah amesema mtu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, alichoma maduka akiwa na lengo la kujipatia faida kupitia bima yake ya biashara.
Kamanda Issah amesema mtuhumiwa huyo alifanya hivyo baada ya kuhamisha biashara yake ili anufaike na bima aliyokuwa analipia.
“Alifanya hivyo kwa tamaa zake binafsi, kwa maono yake na alifanya akijua hatagundulika, mtu huyo ni mmiliki wa kibanda kimojawapo cha biashara katika maduka hayo, alitaka kujipatia faida lakini sasa imegeuka hasara,” alisema.
Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoani humo, Loti Madauda kwa niaba ya Kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji wa mkoa huo alisema tukio hilo lilitokea Aprili Mosi, mwaka huu majira ya saa tatu usiku.
Madauda amesema maduka 21 yaliteketea kwa moto na fremu 89 kati ya 110 ziliokolewa.
Wakati huo huo polisi mkoani hapa wamewakamata watu watatu wakituhumiwa kuvunja ofisi ya mdhibiti wa elimu wilaya na kuiba vifaa vilivyokuwemo ofisini humo.
Kamanda Issah amesema watuhumiwa hao ni Dickson Mwabena (23), Eliud Swale (24) na Agano Komba (24).
Amesema watuhumiwa hao baada ya kuvunja ofisi waliiba vitendea kazi ikiwemo kompyuta na vifaa vingine.
Aidha, Kamanda Issah amesema watu wengine wanne wanashikiliwa kwa kosa la kuiba kwa kushusha mizigo kwenye magari katika barabara kuu ya Njombe -Songea.
Amesema watuhumiwa hao ni Kelvin Mleiwa (34), Godfrey Mginda (24), Ibrahim Ezekiel (24) na Faustine Mvile (24).