NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, amezitaka taasisi za fedha nchini kubadili mtazamo katika utoaji wa mikopo kwa kuangalia zaidi historia ya uaminifu wa wakopaji badala ya kutegemea dhamana ambazo wananchi wengi, hususan wanawake na vijana, hawana.
Amesema mfumo wa sasa wa utoaji wa mikopo bado unaacha nyuma mamilioni ya Watanzania wenye uwezo wa kufanya biashara na kurejesha mikopo kwa sababu hawamiliki mali kama nyumba, ardhi au magari yanayotambulika kama dhamana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Juni 12,2026 katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Rais Samia amesema wanawake na vijana wengi wamekuwa wakikosa fursa za kifedha licha ya kuwa na biashara zinazofanya vizuri na rekodi nzuri za miamala.
“Wanawake na vijana wengi hawana hati za nyumba, hawana ardhi wala magari. Lakini wana biashara, wana historia nzuri ya mauzo, wana kumbukumbu za miamala zinazoaminika na wana uwezo wa kurejesha mikopo. Hawa nao wafikirieni,” amesema
Amesema kuwa benki na taasisi nyingine za kifedha kuwa wabunifu zaidi katika kutafuta mbinu mbadala za kutathmini uwezo wa wakopaji ili kuwajumuisha wananchi wengi zaidi katika mfumo rasmi wa fedha.
Katika msisitizo wake, Rais Samia amesema uaminifu wa mkopaji unapaswa kutambuliwa kama mali muhimu inayoweza kutumika katika maamuzi ya utoaji wa mikopo.
“Tusimnyime mtu mkopo kwa sababu hana mali tulizozoea kuzitambua kama dhamana wakati historia yake inaonesha wazi kuwa anaaminika. Uaminifu ni dhamana kubwa kuliko hata mali inayoonekana,” amesema
Rais Samia pia ametoa changamoto kwa Benki Kuu ya Tanzania na taasisi zote za fedha kujenga mfumo unaomwezesha Mtanzania kubeba historia yake ya uaminifu wa kifedha popote anapokwenda.
Kwa mujibu wa Rais, mfanyabiashara ambaye amekuwa na historia ya biashara na malipo mazuri kwa miaka kadhaa anapaswa kuwa na njia rahisi ya kuthibitisha uwezo wake wa kukopa hata kama hana dhamana za kawaida.
“Mfanyabiashara asiye na hati ya nyumba lakini mwenye historia ya miaka mitano au zaidi ya biashara na malipo mazuri anapaswa kuwa na utaratibu rahisi wa kuthibitisha kuwa anastahili kupata mkopo,” amesema
Amesema hatua hiyo inaweza kufungua milango kwa mamilioni ya wananchi ambao kwa sasa wamebaki nje ya mfumo rasmi wa mikopo licha ya kuwa na uwezo wa kufanya shughuli za kiuchumi kwa mafanikio.
Mbali na suala la mikopo, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali nchini.
Amesema matumizi makubwa ya mifumo hiyo yatasaidia kupanua wigo wa kodi, kuongeza uwazi katika miamala ya kifedha na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Hata hivyo Rais Samia amesema mafanikio ya sekta ya fedha hayapaswi kupimwa kwa kuangalia idadi ya wananchi waliofikiwa na huduma za kifedha pekee, bali kwa kiwango ambacho huduma hizo zimechangia kuongeza kipato cha wananchi, kukuza biashara ndogo na za kati, pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa.
Amesema ni wakati sasa wa kujiuliza maswali muhimu yanayogusa maisha halisi ya wananchi badala ya kutegemea takwimu za upatikanaji wa huduma za kifedha pekee.
“Kipimo chetu kisibaki kuwa wananchi wangapi wamefikiwa na huduma za kifedha, bali tujipime ni kwa kiasi gani huduma hizo zimekuza biashara ndogo ndogo na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi,” amesema
Rais Samia alibainisha kuwa mafanikio ya kweli yanapaswa kuonekana kupitia ongezeko la kipato kwa wananchi, upanuzi wa biashara, upatikanaji wa mitaji kwa wakulima kwa wakati, pamoja na vijana wanaofanikiwa kubadili mawazo yao ya biashara kuwa kampuni zinazozalisha ajira na mapato

