NA MWANDISHI WETU, MWANZA
JESHI la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya mwanaume ambaye hajatambulika kisha mwili wake kuutelekeza pembezoni mwa kilabu cha Pombe kilichopo Kitongoji cha Misheni Wilaya ya Sengerema mkoani humo.
Mauaji ya mwanaume huyo yanadaiwa kutokea usiku wa kuamkia leo April 13, 2023 ambapo mwili wake umekutwa na majeraha usoni na sehemu za siri zikiwa zimetobolewa.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema miongoni mwa wanaoshikiliwa ni mmiliki wa kilabu hicho cha pombe za kienyeji huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi.
“Marehemu amekutwa na majeraha sehemu za paji la uso huku kolodani zikiwa zimetobolewa. Jeshi la Polis liko kazini na litahakikisha linawasaka na litawakamata wote waliohusika na mauaji hayo,”amesema Mutafungwa
Mchungaji wa Kanisa Gospel Rival, James Bukwimba amelaani mauaji hayo huku akisema kuondoa uhai wa mwanadamu mwenzio ni kukinzana na matakwa ya Mungu, akiitaka jamii kumrudia Mungu ili kutokomeza roho ya mauaji.
“Lengo la Mungu ni kuona wanadamu tunasaidiana tofauti na sasa ambapo kumekuwa na matukio lukuki ya watu kuuwana. Tumrejee Mungu kwa kuomba roho ya mauaji itutoke,” amesema Mchungaji Bukwimba
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Misheni yalipotokea mauaji hayo, Hepiphania Damiani amelaani tukio hilo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuwatia mbaroni wote waliohusika huku Mwenyekiti wa kitongiji cha Misheni Joseph Protas, akiwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi.