NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Marekani imetenga kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 1.3 kwaajili ya kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake nchini Tanzania.
Aidha Serikali hiyo imewataka wanawake nchini Tanzania kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kuwania uongozi.
Hayo yamesemwa leo Machi 30, 2023 jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili Ikulu ya Magogoni na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan.
Kamala ambaye aliwasili Ikulu magogoni saa 1:45 mchana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, amesema anaipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwazi wake katika kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Amesema Marekani inatoa fedha hizo ili kuweza kusaidia kukabiliana na changamoto kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake.
”Mahusiano ya Marekani na Tanzania ilianza mwaka 1961 baada ya uhuru wa Tanzania hivyo uongozi wa Rais Biden utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mambo mbalimbali,”amesema.
Aidha amesema kuhusu wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi aliwataka wanawake kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku akimpongeza Rais Samia kwa namna ambavyo anawakomboa wanawake kiuchumi kwani kufanya hivyo kunawafanya wafanikiwe wao na familia zao.
Hata hivyo amesema Marekani itakuwa na mkakati mpya wa ushirikiano kiuchumi na Tanzania kutokana na mwenendo mzuri wa masuala ya utawaala bora na usimamizi wa haki za binadamu kwani ni vitu ambavyo vinamchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Kamala amesema uongozi bora uleta utulivu, usalama na utawala wa sheria ambao wawekezaji na wafanyabiashara wengi uzingatia kabla ya kuweka mitaji yao.
“Ili kuweza kuimarisha hayo na kukuza ushirikiano wetu wa kiuchumi benki ya mauzo ya Kimarekani(Export- import Bank ya Marekani )itasaini hati ya makubaliano na Tanzania ambayo itawezesha upatikanaji wa fedha zitakazopelekwa katika maeneo ya usafirishwaji ,miundombinu ,teknolojia ya kidigitali ,nishati salama na usalama wa kimtandao,”amesema.
PIA SOMA:
USAID yaipatia Tanzania msaada wa Tsh. Trilioni 2.5
Amesema kuwa kuna kazi kubwa inaendelea nchini Tanzania ya kujenga kiwanda cha kwanza barani afrika cha kuchakata madini ambayo yanatumika kwenye betri za magari ya kielektroniki mkakati ambao utawezesha dunia kupata betri zenye madini kutoka Tanzania ifikapo mwaka 2026.
Akizungumzia kuhusu Demokrasia Kamala amepongeza Rais Samia kwa namna ambavyo ameendelea kuimarisha Demokrasia,Utawala bora na Uhuru wa Vyombo vya Habari tangu alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita.
”Umekuwa muwazi umeruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa,uhuru wa vyombo vya habari na hivi karibuni umeshiriki mkutano wa upinzani hii inaonyesha dhahiri kuwa Tanzania inautawala bora,”amesema na kuongeza
”Mbali na hayo Rais Samia katika utawala wake ameweza kuimarisha sekta binafsi,”amesisitiza
Makamu huyo wa Rais amewasili nchini Tanzania Machi 29,2023 majira ya usiku akitokea nchini Ghana na baada ya kukamilisha ziara yake Tanzania anaelekea Zambia ikiwa ni ziara yake ya kwanza barani afrika tangu aliposhika nyadhifa hiyo Mwezi Januari 2021.