NA MWANDISHI WETU
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Yanga leo saa moja jioni inashuka katika dimba la Mkapa kutafuta alama tatu dhidi ya Real Bamako ya Mali.
Meneja Mawasiliano wa klabu hiyo, Ally Kamwe, akizungumzia mchezo huo alibainisha kwamba maandalizi yamekalimika na wanaamini wanakwenda kupata alama tatu wakiwa nyumbani na kujiweka kwenye mstari sahihi wa kutinga hatua ya makundi.
Hivyo aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuongeza hamasa katika mcezo huo ambao kwao ni muhimu kupata ushindi na si vinginevyo kwa kuwa wanacheza katika ardhi ya nyumbani.
“ Maandalizi yako sawasawa kikubwa ni kuomba Mungu wachezaji wetu wawe fiti wakati wa mchezo huo jambo litakalosaidia kufanya vizuri,” amesema.
Yanga inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliochezwa nchini wiki moja iliyopita na baada ya mchezo wa leo Yanga itashuka tena dimbani kwa Mkapa dhidi ya US Monastir ya Tunisia Machi 19 mwaka huu.