NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Kimataifa la Haki Miliki, World Intellectual Property Organization (WIPO), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela(NM-AIST) wamezindua mradi wa mwaka mmoja wa kutumia teknolojia za kanzidata za WIPO ambazo zimekwisha muda wake ili kufanya tafiti katika mkoa wa Njombe.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya uchumi, hususan katika sekta za kilimo na ufugaji.
Amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kuimarisha sekta za kilimo na ufugaji nchini.
Aidha unalenga kutambua, kuchambua na kuhamisha teknolojia ambazo muda wake wa ulinzi wa hakimiliki umeisha kupitia kanzidata za WIPO, ili ziweze kuboreshwa kulingana na mazingira na mahitaji ya Tanzania kwa manufaa ya wakulima, wafugaji na sekta ya viwanda.
Alisema mradi huo utawezesha wataalamu na wabunifu wa ndani kupata teknolojia sahihi zinazoweza kuboreshwa na kutumika katika uzalishaji wa chakula cha mifugo, uchakataji wa mazao pamoja na maendeleo ya viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo.
Amesema Teknolojia hizo zitafanyiwa maboresho kulingana na mahitaji ya ndani na kutumika kuandaa mifano ya mashine na vifaa vitakavyosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa za kilimo,” alisema Dk. Nungu.
Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kupunguza utegemezi wa teknolojia ghali kutoka nje ya nchi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mchango wa ubunifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Pia alisema kabla ya mradi huo kuanza watafanya warsha ya siku tano ili kuwapa mwelekeo wa kukamilisha mchakato huo wadau mbalimbali wa Kilimo ili kwenda kutekeleza mpango huo na ukifanikiwa utasambaa kwenye mikoa mingine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Loy Mhando, alisema mradi huo utasaidia kutumia taarifa zilizopo katika kanzidata za kimataifa za hakimiliki kutafuta teknolojia zinazoweza kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji.
Alieleza kuwa maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni pamoja na teknolojia za uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo, hatua ambayo itasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na kuboresha uzalishaji katika sekta ya mifugo nchini.
Naye mkulima wa mazao ya Parachichi wa mkoani Njombe, Anna Upendo, amesema kuwa tayari kupokea teknolojia hiyo kwa ajili yao wakulima ili kuongeza thamani ya mazao jambo litakalosaidia kupiga hatua zaidi na yuko tayari kuwa balozi wa mchakato huo.
“Nitakwenda kuhamasisha wakulima wenzangu namna ya kutumia teknolojia itakayoletwa na wataalamu wetu itakayosaidia kutumia malighafi za palepale kwetu jambo litakalifanya kupunguza gharama katika ulimaji wa mazao,” amesema.






