NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WACHAMBUZI wa soka kupitia kurasa zao za mitandaoni wameikatia tamaa klabu ya Simba kufanya vizuri katika michezo ijayo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kutokana na kiwango ambacho inakionesha kwa sasa.
Shafii Dauda mchambuzi kutoka Clouds FM amesema, Simba imepoteza uwezo wake wa kusaka matokeo mazuri katika uwanja wa Mkapa na kinachosababisha kushinda ni Bahati tu na si vinginevyo ikiwamo na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
Pia mchambuzi wa michezo wa radio ya EFM, Jemedari Said amesema kuwa Ukweli mchungu ni kwamba Mnyama kachoka na hawezi tena kuonesha maajabu yake yaliyozoeleka katika m ichuano hiyo. Imani ya mshabiki kwa Simba ni kubwa katika haya mashindano ingawa naamini ipo siku watabadilika.
Pia mchambuzi mwingine akinukuliwa kupitia mitandao ya kijamii Abissay Stephen Jr, amesema kwamba Nimemuangalia Chama ameonesha uwezo mkubwa katika kuisaidia timu yake kupata ushindi lakini nimeingalia Simba sijaona mchezo mzuri na hii ni Vipers FC je kwa Horoya itakuwaje?
Licha ya matokeo hayo huku wachambuzi wakisema yao, Meneja wa Mawasiliano wa klabu hiyo Ahmed All, alisema Simba katika mchezo huo ilicheza kimkakati ili kuhakikisha inapata alama tatu nyumbani na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga hatua inayofuata.
“Huenda mpira haukuvutia machoni mwa mashabiki na wadau wa mpira katika michezo hii miwili dhidi ya Vipers FC lakini Simba imecheza kimkakati ili kupata matokeo mazuri na si vinginevyo na sasa tunajipanga kushinda dhidi ya Horoya na ndio mechi inayokwenda kuandika historia”, amesema.
Simba baada ya kuzoa alama sita kwa Vipers kwa kushinda nyumbani na ugenini imefikisha alama hizo na kushisha nafasi ya pili na imesalia na michezo miwili mkononi dhidi Horoya FC ambayo jana ilipoteza dhidi ya Raja na inashika nafasi ya tatu na alama za nne.
Mchezo mwingine ambayo imesalia nao ni dhidi ya Raja ambao wamenekana wababe wa kundi C baada ya kushinda michezo yote minne hadi sasa na kukaa kileleni ikiewa na alama zake 12 na nafasi ya mwisho imekaliwa na Viper yenye alama moja katika michezo minne ambayo imeshacheza.
Hivyo Simba inatakiwa kushinda mchezo ujao dhidi ya Horoya ili kujihakikishia kupata nafasi ya kutinga robo fainali na ikipoteza au ikitoa sare itakuwa imejiweka katika mazingora magumu kwenda hatua inayofuata.