NA JANETH JOVIN
HATIMAYE mtembea kwa miguu aliyegongwa na basi la abiria la ‘Mwendokasi’ wiki iliyopita ambaye ndiye majeruhi pekee wa ajali hiyo aliyesalia katika Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI) ametambulika .
Mtu huyo ambaye ni mwanamme ametambuliwa kwa jina la Osam Milanzi mkazi wa Manzese Midizini jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi amesema kuwa utambuzi huo umefanywa na mke wa majeruhi huyo aitwaye Isha Mohamed pamoja na mdogo wa Osam, Shabani Milanzi.
Mvungi amesema afya ya Milanzi imeimarika kutokana na kazi kubwa inayofanywa na madaktari, viongozi na watumishi mbalimbali wa MOI tangu alipofikishwa hospitalini hapo.
“MOI tunatoa shukrani za dhati kwa vyombo vya habari na watanzania wote kwa ujumla wenye mapenzi mema ambao walishirikiana nasi kutangaza habari za kuwatafuta ndugu wa Milanzi” amesema Mvungi
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya MOI iliyotolewa jana, ilieleza kuwa afya ya majeruhi huyo imeimarika na kwamba ametolewa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa sasa mgonjwa huyo anaweza kuona, kuzungumza, kutaja jina moja tu la Osam hivyo waliomba ndugu, jamaa na marafiki wajitokeze ili kuweza kushirikiana nao kumuhudumia na kwamba anahitaji faraja.
Ajali hiyo ya mwendokasi ilitokea Februari 22, 2023 saa 6:10 mchana katika makutano ya barabara ya Morogoro na Jamhuri, Kisutu Dar es Salaam ikihusisha basi lenye namba T122 DGW aina ya Dragon mali ya kampuni ya UDART.
Basi hilo lilikuwa likitokea Kivukoni kwenda Kimara ambalo liligongana na gari ndogo lenye namba T978 DHZ aina ya Toyota Avanza mali ya Shirika la Ndege la Rwanda.