NA MWANDISHI WETU, DODOMA
KATIKA mfululizo wa kukutana na Idara na Vitengo vya Utalii Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi amekutana na Idara ya Utalii katika ofisi za Wizara hiyo mjini Dodoma februari 25, 2023.
Idara hiyo ina dhamana ya maendeleo na utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali hasa Bodi ya Utalii (TTB) na hata wadau wengine wa sekta binafsi.
“Kazi hapa imefanyika lakini lazima sasa mikakati yetu ya kutangaza utalii isiwe ya kinyonge kama tena kuandaa kalenda, sijui fulana na vitu vidogo kama hivyo pekee; twende viwango vya Royal Tour ambayo Mhe Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan alijitoa akawekeza fedha na muda wake ndio leo inatulipa kwa watalii kumiminika hapa nchini,” amesema Dk Abbasi.
Mbali ya kuitisha kikao cha pamoja cha kimkakati mwezi ujao kati ya Idara hiyo na Bodi ya Utalii, Dk Abbas pia amewataka watendaji wa Idara hiyo kujipanga na kujiongeza ipasavyo kwani katika siku zijazo Wizara hiyo na nchi kwa ujumla inakwenda kutekeleza mkakati mkubwa sana wa kuitangaza nchi na vivutio vyake kama ilivyokuwa kwa uwekezaji na viwango vya Royal Tour.