NA MWANDISHI WETU, MBEYA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema tatizo kubwa linalochelewesha maendeleo katika nchi yetu limetokana na mfumo mbovu wa uongozi wa chama kilichopo madarakani.
Aidha Taifa limeendelea kuwa masikini kutokana na mfumo wa kijamaa ambao wakati wa utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere nchi ilikuwa ikijitawala kijamaa lakini kwasasa hata viongozi waliopo madarakani hawajielewi wanatawala kwa mfumo upi .
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Freeman Mbowe katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani hapa februari 25, 2023.
Amesema kutokana na kutokuwa na katiba mpya kila mpango wa maendeleo nchini kwetu unasimamiwa na serikali kuu ndio maana katiba mpya inahitajika
Mwenyekiti Mbowe amesema mabadiliko ya Katiba ni lazima ili kubadilisha mfumo wa utawala utakaoruhusu viongozi wote kuchaguliwa na wananchi.
Amesema lengo ni kuwa na viongozi wanaojali wananchi ili kupeleka madaraka katika Serikali ya wananchi na wawe huru kuamua hatima ya maisha yao.
“Katika nchi za wenzetu kama Kenya hakuna kiongozi wa Serikali asiyetokana na kura za wananchi, iwe gavana anachaguliwa na wananchi. Ndio maana tunasema katika mabadiliko ya msingi ya sera zetu, lazima viongozi wote watokane na kura za wananchi,” amesema Mbowe
Amesema mfumo uliopo hivi sasa wa kila kitu lazma kibali kitoke Dodoma jambo ambalo linachelewesha maendeleo.
Ameeleza kuwa kutokana na hilo Chadema inaitaka serikali kugatua madaraka hususani katika miradi ya maendeleo.
Akitolea mfano wa Waziri wa Kilimo Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa Hussein Bashe aanasimamia miradi yote ya kilimo jambo ambalo aliita ni ujinga na hata kama waziri huyo angekuwa malaika asingeweza.
Ameeleza kuwa iwapo Chadema itashika Dola itahakikisha inaachana na mfumo wa utitiri wa wilaya na badala yake kutakuwa na Kanda na Majimbo.
Katika hatua nyingine Mbowe amebainisha kuwa baadhi ya viongozi watapigiwa kura badala ya utaratibu uliopo hivi sasa wa uteuaji viongozi.
Amekwenda mbali zaidi na kuainisha kuwa kutokana na sera hiyo ya Chadema itawezesha kila eneo kujitawala kiuchumi kutokana na kukusanya kodi zake na kuwa na waziri wake.
Katika hatua nyingine Mbowe amemshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mikutano ya hadhara.
Aidha amewataka askari kuacha kufanya ukatili kwa kutoligeuza Taifa kama Kosovo.
Aidha amewashauri askari kutumia busara na kuacha kutekeleza amri wanazopewa na viongozi wao .
Mkutano huo ambao ni wa kwanza ndani ya miaka mitatu jijini hapa unatarajia kuendeshwa na mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Mbowe.
Mbowe yupo Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo amemaliza ziara yake mkoani Songwe na sasa atakuwa Mbeya kwa siku mbili akihutubia jijini hapa kisha februari 26 kuendelea mji mdogo wa Tukuyu na kisha Mbarali atakapofunga.