NA MWANDISHI WETU,SAINT PETERSBURG, URUSI
TANZANIA imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Urusi katika Sekta ya Madini kwa kuwekeza katika uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi, uhamishaji wa teknolojia za kisasa na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, wakati akizungumza katika Kongamano la Russia-Africa Raw Materials Dialogue, linalofanyika jijini Saint Petersburg, Urusi, kuanzia Oktoba 12 hadi 17, 2026. Kongamano hilo linawakutanisha washiriki zaidi ya 1,000 kutoka mataifa zaidi ya 40 kujadili ushirikiano katika maendeleo na matumizi ya rasilimali za madini.
Dk.Kiruswa amesema ushirikiano huo unapaswa kuleta manufaa kwa pande zote kwa kuimarisha uchakataji wa madini katika nchi zinazozalisha, badala ya kusafirisha madini ghafi nje ya nchi. Ameeleza kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi, ajira, maendeleo ya viwanda na kuongeza mapato ya nchi zinazomiliki rasilimali hizo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhamisha teknolojia na kuwajengea vijana wa Afrika ujuzi katika utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini, akishukuru Serikali ya Urusi kwa kutoa fursa za mafunzo katika teknolojia za kisasa.
Katika hatua nyingine, Dk. Kiruswa amezikaribisha kampuni za Urusi kuwekeza nchini Tanzania na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya madini ambayo tayari zina leseni, akieleza kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wanaozingatia sheria na taratibu za nchi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuzaa matokeo yanayopimika kupitia miradi yenye tija, uongezaji thamani wa madini na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani, ili kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na rasilimali za madini.





