NA EDNA BONDO, KILIMANJARO
NI takriban miaka 21 tangu kuanzishwa kwa mbio za Kili ambazo kila mwaka wadau mbalimbali hukutana mkoani hapa kwaajili ya mbio hizo maarufu Afrika Mashariki.
Mbio hizi pia zimekuwa chachu ya utalii sambamba na ukuaji uchumi kwani zaidi ya watu 11, 000 hukusanyika kwaajii ya tukio hili ambalo hufanyika mara moja kila mwaka.
Pamoja na mambo mengine mbio hizi zimekuwa ni mojawapo ya kichocheo cha ukuaji uchumi kwani ni wakati wa wafanyabiashara kuvuna pesa.
Wafanyabiashara hao ni wale wa migahawa, baa, hoteli, huduma za usafirishaji abiria pamoja na wauzaji wa nguo.
Kutokana na neema hiyo, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa utalii mkoani Kilimanjaro wamefurahishwa na manufaa ya kiuchumi yatakayoletwa na mbio za Kimataifa za Tigo ‘Kili’ Half Marathon zitakazofanyika katika jiji la Moshi, kaskazini mwa Tanzania Februari 26, 2023.
Wakizungumzia jinsi mbio za kimataifa za Tigo ‘Kili’ Half Marathon za kilomita 21 zinazodhaminiwa na kampuni ya mtindo wa maisha inayoongoza Tanzania, Tigo Tanzania zitakavyowasaidia, baadhi ya wafanyabiashara na wadau wa mjini Moshi wanasema wanatarajia mauzo kuongezeka, kupatikana kwa mtandao mpya wa kibiashara na kutambulika na idadi kubwa ya washiriki watakaohudhuria tukio hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli ya Moshi Kibo Palace, Beatrice Laswai, anasema anatarajia kushamiri kwa biashara katika hoteli yake, hasa wageni kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi watakao hitaji malazi.
Anaeleza kuwa kwa miaka kadhaa sasa, Hoteli ya Setways na Kibo Palace zimekuwa zikidhamini hafla hiyo, huku akitoa sifa kwa mbio hizo kuwa zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara zao.
“Hoteli ya Moshi Kibo Palace inatarajiwa kupokea wateja wengi zaidi kuliko kawaida msimu huu, kutokana na mashindani ya riadha ya Tigo ‘Kili’ Half marathon 2023”, Laswai alisema na kuongeza kuwa wameandaa ofa maalum za vinywaji kwa kushirikiana na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambapo watakuwa na tukio maalum linalojulikana kama ‘Happy Hour’ mwishoni mwa wiki wakati wa mbio za marathoni.
Pia anatoa wito kwa wateja wake kutumia huduma za Tigo hususani ‘Lipa kwa Tigo-Pesa-Lipa Kwa Simu’ ambayo haina ada ya miamala badala ya kutembea na fedha tasilimu ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.
Aidha anaeleza kuwa Setways na Moshi Kibo Palace Hoteli wameandikisha jumla ya wafanyakazi wake 70 kushiriki katika mbio za kimataifa za Tigo ‘Kili’ Half International Marathon kwa kuwa wanaelewa umuhimu wa tukio hilo katika kukuza uchumi na kudumisha afya na ustawi wa wafanyakazi wao.
“Wito wangu kwa waandaaji wa mbio hizo ni kuandaa mbio hizo mara nyingi zaidi kwa mwaka badala ya kufanya hivyo mara moja kwa mwaka kwani mkoa wetu unanufaika sana kiuchumi kupitia mbio za marathon”, Laswai anasema.
Kwa upande wao, Mkurugenzi Mkuu wa hoteli maarufu ya Coffee Tree inayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU), Godfrey Massawe, mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli ya Springlands inayomiliki kampuni ya ZaraTours ya mjini hapa, Zainab Ansell, Ofisa kutoka Keys hotels, Abdi Massawe-Meneja wa Hoteli ya Q-Wine ya mjini Moshi walieleza kuwa, mbali na kuongeza wateja katika hoteli zao, wanatarajia pia kupata mitandao mipya ya kibiashara na wateja kutoka nchi mbalimbali watakaoshiriki mbio hizo.
Kwa upande wake, Kaimu Mlinzi Mkuu wa Hifadhi ya (Utalii) katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA), Imani Kikoti anaeleza kuwa mbio za Kimataifa za Tigo ‘Kili’ half Marathoni zinaunga mkono katika kutangaza upekee wa Mlima Kilimanjaro duniani kwa kuwa watu wengi mbalimbali huja kufurahia hafla hiyo.
“Mbali na kukuza biashara katika ukanda wetu, mbio za kimataifa za Tigo ‘Kili’ Half Marathon zinasaidia sana kuutangaza mlima wetu wa Kilimanjaro kwa hata jina la mbio hizi ni ni ‘Kilimanjaro’, jina la kivutio chetu kikuu cha utalii-Mlima Kilimanjaro ambao pia unajulikana kama ‘Paa la Afrika,” Kikoti anaeleza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio za marathon kwenye Nyumba za Hoteli ya Kibo Palace, Katika Manispaa ya Moshi hivi karibuni, Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo alieleza kuwa kampuni hiyo ya mawasiliano imekuwa ikidhamini mbio za Kimataifa za Tigo, Tigo ‘Kili’ International Half Marathon kwa miaka 8 sasa.
Kwa lengo la kuhamasisha utalii wa kimichezo kupitia Mlima Kilimanjaro ambao ni miongoni mwa vivutio vikuu vya utalii nchini.
Akithibitisha dhamira ya Tigo ya kuhamasisha kuishi maisha yenye afya kupitia mbio zijazo za Tigo ‘Kili’ International Half Marathon 2023, Kinabo aliwahimiza watu kutoka nyanja mbalimbali kushiriki katika michezo na burudani ili kudumisha afya bora. Tigo ndio wadhamini wakuu wa mbio za kila mwaka za kilomita 21 za Tigo Kili Half Marathon zitakazofanyika Februari 26 mwaka huu Moshi Mjini.
Kwa mujibu wake, idadi ya washiriki imeongezeka kutoka 4,500 hadi kufikia 6,000 mwaka huu, na kila mmoja kati ya washindi 4,500 wa kwanza katika mbio za kilomita 21 atapata medali ya kumbukumbu, huku washiriki wote wa mbio hizo wakipokea vyeti vya ushiriki.’Kwa mwaka wa nane mfululizo, Tigo inafuraha kuwa sehemu ya mbio za Kimataifa za Tigo ‘Kili’ International Half Marathon zinazowaleta pamoja wanariadha mahiri, wapenzi wa michezo, marafiki na familia katika kusherehekea michezo, afya ya mwili, burudani, utamaduni, utalii, uhifadhi wa mazingira, maisha yenye afya na kumbukumbu za kudumu.
Kwa kuongezea, zaidi ya wakala 6,604 na wafanyabiashara zaidi ya 600 wa Lipa kwa Simu wako tayari kukuhudumia mjini Moshi, hivyo huhitaji kubeba pesa taslimu ” anaongeza.
Akizungumza kwa niaba ya waandaaji, Mkurugenzi wa Mbio hizo, John Bayo anaeleza kuwa, barabara zote zitaelekea Moshi kwa ajili ya mbio za Kilimanjaro Marathon 2023 ambapo zaidi ya wakimbiaji 11,000 walitarajiwa kushiriki katika mashindano hayo ya kifahari.
“Waliojitokeza ni wengi na tunatarajia tukio lingine kubwa na la kusisimua Februari 26, 2023 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi,” inasema taarifa kutoka kwa waandaji”.
Mratibu alithibitisha kwamba safari hii, usajili kwa njia ya mtandao ulifanya kazi vizuri sana huku zaidi ya asilimia 90 ya washiriki katika mbio za kilomita 42 na 21 wamejiandikisha kwa wakati.