NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. John Jingu, amesema kuwa mafunzo ya wanawake katika uongozi yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi yanalenga kuwajengea uwezo kundi hilo ili kuwa viongozi wazuri na wenye kuleta mabadiliko na maendeleo katika maeneo waliyopo.
Dk. Jingu ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Tano la Wanawake katika Uongozi lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) chini ya dhima ya ‘Mchango wa wanawake katika uongozi barani Afrika’.

Washiriki wa kongamano hilo wametoka katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, Afrika Kusini, Namibia, Cameroon, Rwanda, Gambia, Zambia, Nigeria, Liberia, na mwenyeji Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufungua kongamano hilo, Dk. Jingu alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kuwa viongozi wazuri na watu ambao watakuwa na mchango wa maendeleo katika maeneo waliyopo.
Amesema ni ukweli uliyowazi kuwa viongozi wanatengenezwa hivyo Taasisi ya Uongozi inaendeleza adhima hiyo kwa kutoa mafunzo ili kupata wanawake wakaoshika nafasi za juu za uongozi si kwa sababu za kijinsia bali kutokana na uwezo na sifa walizonazo.
“Msingi wa hayo yote haya ni kwamba viongozi wazuri wanatengenezwa, pamoja na kwamba baadhi wanaweza kuwa wamezaliwa na vipaji mbalimbali na uwezo wa kiuongozi, wakitengenezwa na kujengewa sifa zinazoitajika wanaweza kutoa mchango mzuri zaidi wa maendeleo katika maeneo au sekta walizopo,” alisema na kuongeza
“Mafunzo haya ya uongozi ni mazuri kwa sababu yanatoa fursa kwa wanawake kubadilishana uzoefu wao kwa wao pamoja na watu waliopo kwenye nafasi za uongozi, kila mshiriki katika mafunzo haya ana kocha wake ambaye anamlea na kumsaidia,” amesema
Aidha amesema kupitia mafunzo hayo wanatengeneza waleta mabadiliko katika jamii na kwamba wanawake kwa wanaume wakishirikiana katika shughuli za maendeleo basi mafanikio yatakuwa makubwa na changamoto zilizopo katika jamii zitapungua au kuisha kabisa.
Hata hivyo amesema kongamano hilo, ambalo limekua jukwaa muhimu katika kukuza uongozi wa wanawake barani Afrika, limewakutanisha washiriki kutoka serikalini, sekta binafsi, vyuo vikuu, na asasi za kiraia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema programu mpya ya Wanawake katika Uongozi imelenga kuwajengea uwezo wanawake ili wanapochukua nafasi za kiuongozi waweze kuzitumia vyema na hatimaye kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za juu za kisiasa, kiuchumi na kibiashara.
Singo amesema takwimu zinaonesha kwamba mpaka sasa kuna asilimia 33 pekee ya wanawake wanaoshikilia nafasi kubwa za maamuzi duniani na kwamba kwa takwimu walizonazo zinaonesha itachukua 130 kufikia uwiano wa 50 kwa 50 kama kasi hiyo haitaongezeka.
“Taasisi ya Uongozi imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwajengea uwezo ili kupata wanawake wengi wenye sifa za kushikiria nafasi za uongozi baraka Afrika ikiwemo Tanzania,” amesema Singo na kuongeza
“Mwitikio wa wanawake kushiriki mafunzo haya umekuwa mkubwa, miaka ya nyuma tunapotangaza kuanza kwa kodi waliokuwa wanaomba walikuwa kati ya 500 hadi 600, mwaka huu walioomba viongozi kutoka barani Afrika ni 2009 ila waliopata ni 100, kati ya watu hao walioomba wanatoka Botswana, Namibia, Cameroon, Kenya, Uganda, Marekani, Uingereza na Sweden,” amesema Singo
Aidha Singo amesema wamefanya utafiti mdogo na kubaini kuwa wanawake wengi waliopata mafunzo kwao wameongeza uelewa katika masuala ya uongozi, wameendelea kujiamini na kupata mbinu mpya za ufanyaji wa kazi katika maeneo yao.
Ofisa Mipango wa Umoja wa Ulaya, Alessandro Pisani, amesema kongamano hilo limekuwa hatua muhimu katika juhudi za pamoja za kuweka usawa wa kijinsia kama kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Afrika.
Amesisitiza ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Serikali ya Tanzania, na UN Women katika kuvunja vikwazo vya kimfumo vinavyozuia uongozi wa wanawake.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Usawa wa Kijinsia (UN Women), Katherine Gifford, alisema mpango huo wa utoaji mafunzo kwa wanawake ni hitaji la kimaendeleo linalopaswa kutoa matokeo zaidi ya uwakilishi pekee.
“Tunahitaji mifumo endelevu ya kusaidia wanawake kufika katika ngazi za maamuzi,” amesema Gifford.
Kwa upande wake Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Sitting alisema uongozi siyo cheo bali ni kujitambua na kuwa na uvumilivu unapokabiliwa na changamoto hivyo amewataka wanawake wasihofu kuanguka na kwamba wakipatwa na hali hiyo au kukosa walichotamani wanapaswa kusimama tena na kujaribu upya.

