NA VERONICA SIMBA, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na uadilifu ili kuondoa malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wananchi ambayo yanaweza kuichafua Serikali.
Ameyasema hayo jana wakati wa kusaini mikataba ya upelekaji umeme vijijini kupitia Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C na B, lililofanyika katika Ofisi Ndogo za REA zilizoko jijini Dar es Salaam.
Akitoa mfano alisema yapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Wakandarasi wamekuwa wakikata miti katika maeneo yao pasipo kuwapa taarifa, jambo ambalo amelikemea vikali akisema kamwe halikubaliki.
Akieleza zaidi, Mhandisi Saidy aliainisha mambo mengine kadhaa ambayo yanapaswa kuzingatiwa na kila Mkandarasi ikiwa ni pamoja na kutimiza lengo maalumu la Serikali la kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwafikishia huduma ya umeme.
Akifafanua kuhusu suala hilo, Mkurugenzi Mkuu alisitiza kuwa Wakandarasi wote wanaoenda kufanya kazi vijijini wanapaswa kuzingatia kuwa wanafanya kazi hiyo wakiwa ni waajiriwa wa Serikali sawa na mikataba waliyosaini.
Aidha, amewataka kufanya kazi kwa ukaribu na viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali pamoja na Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi katika maeneo husika. Katika hili, amewataka kuhakikisha wanawajibika kwa viongozi hao kwa kuwapatia taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini Tanzania (AFD), Celine Robert, ambao ni mojawapo ya Wafadhili katika miradi hiyo, alisema Ufaransa inafurahishwa kuwa sehemu ya uchangiaji wa miradi inayosaidia kuboresha maisha ya kila siku ya wananchi na akaongeza kuwa watafarijika kuona wakandarasi wakitekeleza miradi hiyo kwa ufanisi.
Naye Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu aliwasisitiza wakandarasi hao kufanya kazi kwa mujibu wa mikataba waliyosaini huku Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu, Mhandisi Advera Mwijage akiwataka kuhakikisha wanawalipa vibarua wao kwa wakati pamoja na kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira.