NA FLORAH AMON, DAR ES SALAAM.

ZAIDI ya miamala milioni 200 yenye thamani ya takribani Sh.Trilioni 70 imefanyika kupitia Mawakala wa Benki ya CRDB nchini kote katika kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha, kati ya kiasi hicho, zaidi ya Sh.Trilioni 3 /-ni makusanyo ya Serikali yaliyopokelewa kupitia mfumo wa uwakala.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 13,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano na Mawakala wa Benki ya CRDB, Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Muhinuliza Buberwa, amesema mafanikio hayo yanaonesha namna huduma za kifedha kupitia mawakala zinavyochangia kukuza ujumuishi wa kifedha na kuongeza mapato ya Serikali.

Buberwa amesema kuwa, kwa sasa Benki ya CRDB ina zaidi ya mawakala 45,000 nchi nzima, sawa na asilimia 55 ya mawakala wote waliopo nchini.
“Kuwepo kwa idadi kubwa ya mawakala ni jitihada kubwa ya Benki ya CRDB, lakini isingewezekana bila uwepo na juhudi zenu ninyi mawakala kwa sasa, miamala mingi inapitia kwenye mfumo huu wa uwakala,” amesema Buberwa.
Aidha, ameongeza kuwa kumekuwa na mapinduzi makubwa ndani ya kipindi cha miaka 12 tangu kuanzishwa kwa huduma za uwakala, hasa katika matumizi ya mifumo ya kidijitali na maboresho ya huduma. Ameeleza kuwa, kwa sasa hakuna tofauti kubwa kati ya mteja anayetembelea tawi la Benki ya CRDB na yule anayetumia huduma kupitia wakala, kwani huduma zote muhimu zinapatikana kwa urahisi kupitia mawakala.

Katika hatua nyingine, Buberwa amesema Benki hiyo imezindua huduma bunifu ijulikanayo kama Tokenization, ambayo itawawezesha wateja wa CRDB hata wale wasio wateja kutoa fedha walizotumiwa kupitia wakala yeyote wa CRDB bila kutozwa gharama ya ziada.

“Huduma hii inamwezesha mteja wa CRDB kutuma pesa kwa mtu yeyote, bila kujali kama ana akaunti ya CRDB au la anatakiwa tu kuingia kwenye simu yake, kuchagua sehemu ya tokeni, kisha kuingiza namba ya simu ya mpokeaji atapokea code ambayo ataenda nayo kwa wakala wetu wa CRDB na atapatiwa fedha zake,” amesema Buberwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawakala na Huduma za Malipo wa Benki ya CRDB, Catherine Lutenge, amesema semina hiyo imewahusisha mawakala zaidi ya 800 kutoka Wilaya ya Ubungo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia mawakala wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.

Mawakala walioshiriki katika semina hiyo wamesema wamepata elimu muhimu kuhusu matumizi sahihi ya mashine za POS, jambo ambalo wamelitaja kuwa litaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma zao za uwakala.


