NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuendelea kutumia Riba ya Benki Kuu (CBR) ya asilimia 5.75 kwa robo ya mwisho ya mwaka inayoisha Disemba 2025.

Akizungumza katila mkutano na viongozi es kibenk pamoja na wanandishi wa habari ya jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba amesema kuwa
kufuatia kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kilichofanyika Oktoba 1, 2025 ambapo Uamuzi huo umetokana na tathmini ya mwenendo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi, ambapo viashiria vinaonesha kuwa uchumi utaendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha huku mfumuko wa bei ukibaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.

Amesema kuwa uchumi wa nchi unaendelea kuimarika licha ya misukosuko ya kiuchumi duniani, na kwamba BoT itaendelea kusimamia sera ya fedha kwa makini ili kuhakikisha uthabiti wa thamani ya fedha na ukuaji endelevu wa uchumi.

Gavana Tutuba ameongeza kuwa utekelezaji wa sera ya fedha katika robo iliyopita ulifanikiwa kuongeza ukwasi katika mabenki, jambo lililosaidia kupunguza riba za mikopo ya muda mfupi baina ya mabenki hadi kukaribia kiwango cha CBR.
Amesisitiza kuwa sera za fedha zimeendelea kuwa chombo muhimu katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea shughuli za kiuchumi.

“Katika soko la kimataifa, uchumi wa dunia ulishuhudia kasi ndogo ya ukuaji kutokana na mvutano wa kisiasa na biashara, lakini benki kuu nyingi ziliamua kutopandisha viwango vya riba ili kusaidia uchumi kuimarika bei ya mafuta ghafi duniani ilipungua hadi wastani wa dola 68 kwa pipa, huku bei ya dhahabu ikiendelea kuwa juu, jambo linalotarajiwa kuimarisha mapato ya fedha za kigeni kwa Tanzania”Amesema Gavana Tutuba
Aidha amebanisha kuwa kwa upande wa ndani, mfumuko wa bei Tanzania Bara ulikuwa asilimia 3.4 mwezi Agosti 2025, ndani ya lengo la taifa na ya mashirikisho ya kikanda ya EAC na SADC. Uhakika wa chakula, utulivu wa shilingi, na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti umechangia kwa kiasi kikubwa kudhibiti mfumuko huo huku Zanzibar nayo ilirekodi mfumuko wa asilimia 4.0, chini ya ukomo wa asilimia 5 unaokubalika.
Tutuba amesema Kwa upande wa shughuli za uchumi ziliendelea kuimarika, ambapo Tanzania Bara ilikua kwa asilimia 5.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, na ukuaji huo ulitegemewa kuongezeka zaidi katika robo ya pili na ya tatu. Zanzibar ilikua kwa asilimia 6.4, huku matarajio ya mwaka mzima yakifikia asilimia 7.3, yakichochewa na utalii, kilimo na ujenzi. Mikopo kwa sekta binafsi nayo iliongezeka kwa asilimia 15.9, ikionesha kuimarika kwa uhusiano kati ya sekta ya fedha na uchumi halisi.
“Sekta ya fedha iliendelea kuonesha ustahimilivu, ambapo mikopo chechefu ilipungua hadi asilimia 3.3 chini ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 5. Shilingi ya Tanzania ilionyesha uthabiti, ambapo thamani yake iliongezeka kwa asilimia 8.4 katika robo ya tatu, na akiba ya fedha za kigeni kufikia Dola za Marekani milioni 6.4, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi mitano.”Ameongeza
Akihitimisha taarifa yake, Gavana Tutuba amesema Kamati ya Sera ya Fedha inatarajiwa kukutana tena Januari 7, 2026, na hivyo CBR mpya kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026 itatangazwa Januari 8, 2026 na kusisisitiza kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza sera zenye kuzingatia uthabiti wa uchumi, maendeleo ya sekta binafsi, na ustawi wa wananchi kwa ujumla.

