NA STELLA GAMA, DAR ES SALAAM
MMOJA wa Madaktari bingwa wachache duniani wanaofanya upasuaji mgumu wa moyo kwa watoto Prof. Tomasz Mroczek kutoka Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland ameipongeza Serikali kwa kusomesha wataalamu wa moyo na kununua vifaa tiba vinavyotumia teknolojia ya kisasa.
N GAMA, DAR ES SALAAM Dar es
Prof. Mroczek alizitoa pongezi hizo hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto waliyoifanya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Prof. Mroczek alisema hii ni mara yake ya kwanza kufika hapa nchini na walikuja kuona namna ambavyo madaktari wa JKCI wanavyofanya upasuaji wa moyo na kuangalia jinsi watakavyoweza kushirikiana katika kufanya upasuaji mgumu zaidi.
“Kitu nilichokitegemea kukikuta siyo nilichokikuta hapa, nimekuta madaktari wanafanya upasuaji mgumu wa kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ambayo haijakaa katika mpangilio wake kwa kutumia muda mfupi tofauti na nchi zingine nilizokwenda pia kuna wataalamu wazuri na vifaa tiba viko vya kutosha na vya kisasa vinavyoenda na teknolojia ya matibabu ya moyo inayotumika katika nchi zilizoendelea”,.
“Nimekutana na watalamu wazuri ambao tumefanya nao upasuaji wa moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ninaamini ushirikiano huu utakuwa endelevu ili sote kwa pamoja tuweze kuwahudumia watanzania wenye matatizo ya moyo”, alisema Prof. Mroczek.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Peter Kisenge aliwashukuru wataalamu hao kutoka nchini Poland ambao walifanya upasuaji mkubwa kwa watoto na mdogo kwa watu wazima na kusema kuwa ujio wao unaenda kufungua milango ya mafunzo kwa madaktari hapa nchini.
Dk. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo alisema kwa muda wa siku tano ambao madaktari hao walikuwepo katika Taasisi hiyo wameweza kufanya upasuaji mgumu wa moyo na kutoa mafunzo na ujuzi kwa wataalamu wa JKCI.
“Tulisaini makubaliano na wenzetu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland ya kushirikiana katika mafunzo, tafiti na kufanya matibabu. Ushirikiano huu umeanza kufanya kazi na utakwenda kufungua milango ya kufanya tafiti mbalimbali zitakazoleta manufaa kwa nchi ikiwepo uingizaji wa fedha za kigeni”, alisema Dk. Kisenge.
“Walipofika wametuonyesha vitu ambavyo kwetu sisi ilikuwa ni vigunu kufanya kwani wamekuja kutuonyesha namna ya kutumia mitambo iliyopo ikiwepo kurekebisha mishipa ya damu kwenye moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Dk. Kisenge alisema kama watoto hao watano waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wangepelekwa kutibiwa nje ya nchi kila mmoja angetumia zaidi ya Sh. Milioni 20 kwaajili ya upasuaji lakini kwa kutibiwa kwao hapa nchini wameokoa zaidi ya Sh. Milioni 100.
Prof. Bartconie Guzlk kutoka Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland ambaye alifanya upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kutumia mtambo wa Cathlab alisema madaktari wa Tanzania wapo tayari kujifunza kwaajili ya kusaidia watu wenye matatizo ya moyo kwani wanafanya kazi kwa bidii na umakini mkubwa.
“Tutaendelea kushirikiana na JKCI katika kufanyakazi ya kuwatibu watu wenye matatizo ya moyo na kufanya tafiti zitakazosaidia katika matibabu, hii ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania nimefurahi na nimeipenda hii nchi ninaahidi tutaendelea kushirikiana zaidi”, .
Awali Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI Dk.Angela Muhozya amesema uwepo wa madaktari hao ambao ni Daktari bingwa wa moyo na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto umetoa fursa kwa wao kujifunza mambo makubwa zaidi katika upasuaji wa moyo.
“Tangu tumeingia nao mkataba ni mwaka sasa na tulipopata nafasi ya kuwatembelea wenzetu katika chuo chao tuliona ni namna gani wanafanya upsauaji wa mishipa ya damu pamoja na moyo tukatumia fursa hiyo kuomba waje nchini ili na sisi tuweze kufaidika,”alisema Dk Muhozya
Naye daktari bingwa wa upasuaji moyo kwa watoto wa JKCI Godwin Sharau alisema uwepo wa madaktari bingwa kutoka Poland umesaidia kwa wao kujifunza zaidi kwani madaktari hao ndani ya siku tatu wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji mkubwa watoto watano ambao ulikuwa mgumu kwa wao kufanya.
“Tumekutana na madaktari ambao tunaamini tunaweza kufika kwenye viwango vya juu kutokana na utendaji wetu na pia kwetu ni fursa kwani Prof. Mroczek anatumiwa na watu wengi duniani katika kusaidia watoto”, alisema Dk.Sharau.