NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema imejipanga kuongeza huduma za usafirishaji baharini kwa kujenga bandari zaidi ikiwemo ya Kizimkazi Wilaya ya Kusini Unguja pamoja na Wete ambayo itakifungua kisiwa hicho na mikoa jirani ya Tanzania Bara, hususani Tanga.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk Khalid Mohamed wakati akishuhudia utiaji saini wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu ya utekelezaji wa miradi miwili ya ujenzi wa bandari ya Kizimkazi na Wete Pemba, katika makao makuu ya wizara, Kisauni Unguja.
Amesema kuwapo kwa bandari ya Kizimkazi ni muhimu kwa ajili ya kuongeza shughuli za usafiri kati ya wananchi wa vijiji jirani katika mkoa huo ambao wamekuwa wakifanya safari kwenda Tanzania Bara.
Mohamed amesema serikali imechukua jukumu hilo ikiwa ni sehemu ya mikakati yake ya kuongeza shughuli za kibiashara kwa wananchi wa pande mbili ili kupata kipato.
“Serikali ya Zanzibar awamu ya nane tumejipanga zaidi kuimarisha huduma za mawasiliano ya baharini ikiwemo ujenzi wa bandari ambao tunaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza shughuli za wananchi kiuchumi,” amefafanua
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Shimari Omar Shomari amesema upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari ya Wete ni muhimu kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kukifungua Kisiwa cha Pemba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Harbour Engineering, Cheng Yong Jian aliomba ushirikiano zaidi kwa taasisi mbalimbali katika kazi za upembuzi yakinifu katika ujenzi wa bandari hizo.
“Napenda kuiahidi wizara kwamba kazi ya upembuzi yakinifu tutaifanya kwa uadilifu na wakati ambao mashirikiano kwa watendaji mbalimbali yanahitajika katika kufanikisha kazi hiyo,” amesema