NA MWANDISHI WETU, GEITA
WATU wawili ambao wametambulika kama wachimbaji wadogo wa madini wamepoteza maisha baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba kinyemela katika mgodi uliokuwa umefungwa uliopo eneo la Bingwa kijiji cha Lwamgasa wilayani Geita.
Waliopoteza maisha ni Elias Joseph ( 25) Mkazi wa Singida na William Mohamed (30) mkazi wa Nyankumbu mjini Geita.
Akizungumza leo Mei 6, 2023 Mwenyekiti wa Kijiji cha Rwamgasa, Musa Musongoma amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo.
Amesema mgodi huo unaomilikiwa na Hussein Mwananyanzara ulikuwa umefungwa na wachimbaji hao wakiwa kundi la watu wanne waliingia kinyemela usiku kwa lengo la kuchimba.
“Usiku tulipata taarifa, wakati tunajitahidi kuwaokoa tulikuta wawili wameshafariki na wengine wawili walikimbia. Utaratibu wa maeneo yaliyofungwa mmiliki anapaswa kufukia mashimo na kuweka kibao cha tangazo na vyote vipo ila hawa wameingia kinyemela,”amesema
Amesema miili ya wachimbaji hao imehifadhiwa Kituo cha Afya Katoro na kuwataka wachimbaji wadogo kuepuka kuingia kwenye maeneo yaliyofungwa kwakuwa yanahatarisha maisha yao.
Mmiliki wa mgodi huo, Hussein Mwananyanzara amesema eneo hilo lilikuwa limefungwa na wachimbaji hao waliingia kinyemela kipindi hiki cha mvua ambapo udongo umejaa maji hivyo kuporomokewa na kifusi.
Akizungumza kwa simu, Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita, Martine Shija amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa watu wake wako njiani kuelekea eneo la tukio na taarifa zaidi atazitoa baadaye.
Kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2023 wachimbaji wadogo 13 wameripotiwa kupoteza maisha mkoani hapa wakiwa kwenye shughuli zao za uchimbaji na 10 kati yao waliingia kinyemela kwenye maeneo yasio rasmi.