NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini (OSHA) umeipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mfano kwa taasisi za fedha katika kuzingatia na kujali usalama na afya kwa wafanyakazi wake.
Aidha, Kwenye kilele cha maadhimisho hayo Benki ya CRDB ilipewa tuzo kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kwa usalama na afya za wafanyakazi wake.
Pongezi hizo zimetolewa na Mtendaji Mkuu wa OSHA Khadija Mwenda kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Morogoro.
Alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuuhamasisha umma kuhusu usalama na afya mambo wanayoyasimamia chini ya sheria namba tano ya mwaka 2003 na kuhakikisha hilo linazingatiwa OSHA imekuwa ikifanya maadhimisho yanayohusisha kuwakumbuka wafanyakazi waliopoteza maisha au kuathirika wakiwa kazini .
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema serikali inatambua na kuthamini usalama na afya mahali pa kazi.
Waziri Ndalichako alisema kutokana na hilo serikali kupitia OSHA inaendelea kusimamia kwa karibu sheria namba tano ya afya na usalama mahali pa kazi ya mwaka 2003 kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi kutopata ajali au kuambukizwa magonjwa.
Mkuu wa kitengo cha Ulinzi, Usalama na Mwendelezo wa Biashara wa Benki ya CRDB, Misana Mutani alisema ufanisi mzuri wa benki hiyo ndiyo uliozaa matunda ya wao kupewa tuzo tatu katika kuzingatia afya na usalama mahali pa kazi kwa wafanyakazi.
Mutani alisema CRDB sio tu inazingatia usalama wa wafanyakazi wake pekee bali jamii inayowazunguka kwa maana ya wateja na wageni wanaotembelea maeneo ya benki hiyo kwani inahakikisha wapo salama wakati wote.
Naye Meneja na Usaidizi wa Huduma wa CRDB, Elia Mnonjela alisema wakati anaongea na wadau waliotembelea banda lao katika maonyesho hayo wamefahamishwa kuhusu huduma nafuu zinazowapa fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Kwenye maadhimisho hayo Benki ya CRDB ilitunukiwa tuzo tatu. Ya kwanza ni mshindi wa kwanza katika kundi la benki na taasisi za fedha katika utekelezaji wa sera za Osha. Tuzo nyingine ni ya ufanisi katika utoaji huduma bora unaozingatia afya na usalama wa kazi kwa benki na ile ya kamati bora ya Osha katika huduma za kibenki.