NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Mifupa Muhimbili(Moi) imesema hali ya mwanaume ambaye video yake imesambaa mtandaoni ikionesha namna alivyogongwa na basi mwendokasi mapema jana asubuhi eneo la Kisutu jijini Dar es salaam bado sio nzuri.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Moi Patrick Mvungi , mwanaume huyo bado hajatambulika na hadi sasa hajitambui.
Mvungi amesema mwanaume huyo yupo chini ya chumba cha uangalizi maalum( ICU ) akiendelea na matibabu baada ya kupata majeraha makubwa kichwani.
Mbali ya hayo Mvungi ameiambia Demokrasia kwa njia ya simu kuwa jitihada za kuokoa maisha ya mwanaume huyo zinaendelea kufanywa na madaktari bingwa wa Moi.
Hata hivyo Mvungi amesema baadhi ya majeruhi wamesharuhusiwa na kuahidi kuendelea kutoa taarifa kadri inavyohitajika.