NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo manne muhimu, likiwemo la kuitaka Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam unatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaozingatia viwango vya kimataifa.
Mbali na hilo, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Nishati kuimarisha akiba ya kimkakati ya mafuta ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kimataifa pamoja na mabadiliko ya bei katika soko la dunia.
Rais ameyasema hayo leo Jumanne Machi 3, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, akisisitiza kuwa wakandarasi na washauri elekezi wanapaswa kuzingatia ubora, weledi na kasi katika utekelezaji wake ili Serikali na wananchi wanufaike kikamilifu na uwekezaji huo mkubwa.
Aidha, ameiagiza TPA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa vipimo na shehena za mafuta kuanzia yanaposhushwa hadi hatua ya usambazaji, kwa lengo la kuongeza uwazi na kulinda mapato ya taifa.
“Lakini kama nilivyosema siku zote, suala la mifumo kusomana ni muhimu ili kusiwe na mianya ya upotevu wa mapato ya taifa,” amesema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa mradi huo unapaswa kujengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama ili kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu imara cha biashara ya nishati katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hata hivyo Rais Samia amesema kuwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya uchukuzi yameleta mageuzi chanya katika utendaji wa bandari nchini, hatua itakayowezesha kupokea na kuhudumia meli kubwa zinazofanya safari katika bandari kuu za kimataifa.
Amesema kuwa uwekezaji huo utaongeza ufanisi wa huduma za upakuaji na upokeaji mizigo, jambo litakalofanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Kutokana na mafanikio hayo, mapato ya serikali kupitia kodi ya forodha yameongezeka na kufikia zaidi ya Sh. Trilioni 12, hatua inayoongeza uwezo wa serikali kugharamia miradi ya maendeleo na kuimarisha uchumi wa taifa.,” amesema
Rais Samia ameeleza kuwa ushirikishaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari umekuwa mkakati wa kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Kupitia mfumo huo, TPA imefanikiwa kupunguza mzigo wa gharama za moja kwa moja za uendeshaji na kuelekeza nguvu katika uwekezaji wa miundombinu mipya.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa kasi ya maendeleo katika sekta ya bandari imeongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, na kwamba utekelezaji wa mipango ya maendeleo kuelekea Dira ya 2050 unaendelea kwa mafanikio makubwa kupitia ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo wa miundombinu ya upakuaji na uhifadhi wa mafuta kutaiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa kinara wa huduma hizo katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Profesa Mbarawa amesema Wizara ya Uchukuzi imejikita katika kuimarisha huduma za bandari kwa kuboresha mnyororo wa usafirishaji na usambazaji wa mizigo, hatua inayolenga kupunguza msongamano uliokuwa ukiikumba Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Ameeleza kuwa maboresho yanayoendelea yameanza kuleta matokeo chanya, ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya upakuaji na upakiaji wa mizigo, kupungua kwa muda wa meli kukaa bandarini, pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Amesisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya uchukuzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema hadi kufikia Machi 2, 2026, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 41, na kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika Februari 2027.
Mbossa amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji na usambazaji wa mafuta nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Miongoni mwa manufaa yanayotarajiwa ni kupungua kwa muda wa upakuaji wa mafuta kutoka wastani wa siku 22 za sasa hadi siku saba pekee, hatua itakayopunguza msongamano wa meli bandarini.
Ameongeza kuwa mradi huo utaondoa tatizo la uhamishaji wa mafuta kwa njia ya mileti kutoka kwenye gati, pamoja na kuondoa tozo ya ucheleweshaji wa upakuaji mafuta ambayo kwa sasa hufikia wastani wa shilingi milioni 28 kwa kila meli kwa siku.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema hadi kufikia Machi 2, 2026, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 41, na kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika Februari 2027.
Mbossa amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji na usambazaji wa mafuta nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Miongoni mwa manufaa yanayotarajiwa ni kupungua kwa muda wa upakuaji wa mafuta kutoka wastani wa siku 22 za sasa hadi siku saba pekee, hatua itakayopunguza msongamano wa meli bandarini.
Ameongeza kuwa mradi huo utaondoa tatizo la uhamishaji wa mafuta kwa njia ya mileti kutoka kwenye gati, pamoja na kuondoa tozo ya ucheleweshaji wa upakuaji mafuta ambayo kwa sasa hufikia wastani wa Sh. Milioni 28 kwa kila meli kwa siku.
Amesema hali hiyo inatarajiwa kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kimataifa, na kuifanya kuwa kitovu muhimu cha biashara ya mafuta katika ukanda huo.





