NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
HIFADHI ya Taifa ya Kilimanjaro, (KINAPA) kuadhimisha ya Miaka 50 tokea kuanzishwa kwake, (Golden Jubilee), Machi 16, 2023 ambapo mgeni resmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Aidha wadau zaidi ya 500 wanatarajiwa kushiriki zoezi la kusafisha mlima huo kwenye njia zote sita sanjari na zoezi la kupanda miti ya asili kwenye eneo la Usseri.
Hayo yameelezwa na Naibu kamishna wa Uhifadhi, Herman Batiho anayehusika na masuala ya Uhifadhi na Maendeleo ya biashara na Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Angela Nyaki wakati wakizungunza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Hifadhi za Taifa nchini,(TANAPA) jijini Arusha
Batiho amesema maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyikia makao makuu ya hifadhi hiyo yaliyo kwenye lango la Marangu ambapo yatatanguliwa na shughuli mbalimbali zenye lengo la kuzidi kuitangaza hifadhi hiyo kitaifa na kimataifa.
“Tunataka kuihakikishia dunia kwamba mlima Kilimanjaro upo eneo la Tanzania na kuonyesha maendeleo ya utalii kwa mlima Kilimanjaro tangu hifadhi ilipoanzishwa na hadi leo hii tunafikia miaka 50 tumepita katika vipindi mbalimbali vya utalii,” amesema Batiho.
Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro, Nyaki amesema maadhimisho hayo yatatanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo kufanya usafi wa mlima, kongamano na upandaji miti.
Amesema kuwa wanatarajia kuanza usafi wa mlima kuanzia Machi mosi mpaka 10, 2023 ambapo wanatarajia wadau 500 watashiriki.
“Mlima utasafishwa wadau watapanda njia zote sita ambapo wadau hao watakuwa katika makundi mawili moja likiwa linasafisha mlima na lingine likiwa linashusha taka zilizokusanywa,” amesema Nyaki na kuongeza
… zoezi hilo litaenda sanjari na utoaji wa elimu ya kusafisha mlima. Zoezi hili huwa tunalifanya siku zote huwa tunahimiza wanaopanda mlima kuhakikisha wanauacha ukiwa msafi”.
Nyaki amesema pia kutakuwa na shughuli ya ugawaji na upandaji miti ndani ya hifadhi eneo la Usseri ambapo mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ataongoza zoezi hilo.
Akieleza sababu za kuchagua eneo la Usseri Mhifadhi huyo amesema kuwa eneo hilo ambalo liko wilayani Rombo limeathirika sana na mimea vamizi na tayari walishaondoa baadhi ya miti hiyo hivyo kwa sasa wanafanya zoezi la kurudishia miti ya asili.
Nyaki amesema kuwa Machi 15, 2023 wanatarajia kuwa na mdahalo kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambapo mada zitakazojadiliwa ni pamoja na uhifadhi, utalii na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkuu huyo wa Hifadhi ya Kilimanjaro, amesema kuwa pia watawatembelea waongoza utalii wa miaka ya 1970 na 1980 kupata taarifa kutoka kwao juu ya hali ilikuwaje kipindi kile ukilinganisja na sasa, hasa kwenye masuala ya mavazi na miundombinu.
“Pia tutawatembelea na wahifadhi wetu waliowahi kukaa hifadhi ya Kilimanjato kipindi cha nyuma. Watatupa na wenyewe uzoefu wao tujue tulipotoka tulipo na tunapoelekea,” amesema Nyaki.
Amesema kuwa wadau watakaotaka kushiriki mazoezi hayo wanaweza kuingia kwenye tovuti ya TANAPA (www.tanzaniaparks.go.tz) kwa ajili ya kujisajili.