NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imeanza kutekeleza programu maalumu ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia mfumo wa akaunti binafsi za wanafunzi (SIPA), ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kusimamia fedha zao na kujiandaa na maisha ya kujitegemea.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema programu hiyo ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuwawezesha vijana kupata maarifa ya kifedha na stadi za kusimamia fedha binafsi wakati wa masomo na baada ya kuhitimu.
Akizungumza katika uzinduzi wa programu hiyo, Tutuba amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa Mei mwaka huu jijini Dodoma kati ya BoT na HESLB, ambayo sasa yameanza kutekelezwa kupitia mfumo wa kidijitali.
Amesema elimu ya fedha ni muhimu kwa kila Mtanzania, wakiwemo wanafunzi wanaopata mikopo ya elimu ya juu, wazazi, walezi, wafadhili na wadhamini wa masomo, kwa kuwa inawawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi na usimamizi wa fedha.
Tutuba amesema kupitia ushirikiano na HESLB, BoT imeandaa maudhui maalumu ya elimu ya fedha yaliyowekwa katika kitabu kitakachopatikana kupitia tovuti ya benki hiyo, tovuti ya HESLB na mfumo wa SIPA ili kuongeza wigo wa wanafunzi na wadau wengine kupata maarifa hayo.
Ameongeza kuwa programu hiyo haitawanufaisha wanafunzi wanaopata mikopo pekee, bali pia wale wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu bila mikopo, pamoja na wanaotarajia kuanza masomo yao ili wapate elimu hiyo mapema kabla ya kuanza maisha ya chuo.
Kwa mujibu wa Tutuba, maudhui ya programu hiyo yamejikita katika maeneo muhimu ya usimamizi wa fedha, yakiwemo kupanga bajeti, kuweka akiba, uwekezaji, kukopa kwa tija, kujilinda dhidi ya utapeli wa kifedha na kutafuta vyanzo halali vya kipato.
Tutuba amesema programu hiyo pia inalenga kuwajengea vijana uwezo wa kukuza ujuzi na ubunifu, pamoja na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika sekta tofauti nchini.
Amesema elimu ya fedha itawasaidia wanafunzi kuelewa umuhimu wa kupanga bajeti kwa kuainisha vyanzo vya mapato na matumizi kulingana na vipaumbele vyao, ili kuhakikisha fedha wanazopata zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ameeleza kuwa suala hilo ni muhimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kuwa linawawezesha kuelekeza fedha wanazopata katika mahitaji muhimu ya masomo na maisha yao ya kila siku, ili waweze kusoma vizuri, kufaulu na kuhitimu kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia amesema programu ya elimu ya fedha kwa wanafunzi na wanufaika wa mikopo itasaidia kuwajengea vijana uwezo wa kusimamia fedha zao, kupanga matumizi na kuweka akiba, huku ikichangia kuimarisha urejeshaji wa mikopo.
Dk. Kiwia, amesema jukumu la bodi hiyo haliishii katika kutoa mikopo na ufadhili wa elimu ya juu kwa vijana wenye sifa na mahitaji, bali pia kuwajengea uelewa wa matumizi sahihi ya fedha.
Amesema elimu ya fedha ni muhimu kwa vijana kwa kuwa itawasaidia kusimamia fedha zao vizuri wanapokuwa masomoni na hata baada ya kuhitimu na kuingia katika soko la ajira.
Dk. Kiwia amesisitiza programu hiyo inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya HESLB na BoT, inalenga kuwafikia wanafunzi na wanufaika wa mikopo pamoja na jamii kwa ujumla, kwa kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, kupanga matumizi, kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kutumia huduma rasmi za kifedha.
Amesema elimu hiyo itasaidia vijana kuepuka changamoto zinazoweza kusababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya fedha, huku ikiwajengea uelewa kuhusu mikopo kama nyenzo ya kuwawezesha kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha, amesema elimu ya fedha itasaidia kuimarisha uelewa wa wanufaika kuhusu wajibu wa kurejesha mikopo kwa wakati, hatua itakayosaidia kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kutumika kuwawezesha wanafunzi wengine kupata elimu ya juu.







