*Asisitiza kuhusu mazoezi ya mwili ili kujikinga na maradhi yasiyoambukiza
*Apongeza NBC Dodoma Marathon kuiunga mkono Serikali mapambano
dhidi ya Saratani Shingo ya kizazi
NA MWANDISHI WETU,DODOMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko amesema
kuwa asilimia 80 ya vifo nchini vinaweza kuzuilika endapo Watanzania
wataamua kubadili mtindo wa maisha ikiwemo kuwa na utaratibu wa
kufanya mazoezi ya mara kwa mara.
Amesema hayo leo Jumapili Julai 27 ,2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kilele cha msimu wa Sita wa
NBC Dodoma Marathon 2025 ambayo imelenga kukusanya fedha kwa ajili ya
kuokoa afya ya mama na mtoto.
“Taarifa ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2022, inaeleza kuwa,
mazoezi ya mara kwa mara kama vile kukimbia, yana uwezo wa kupunguza
hatari ya ugonjwa wa moyo kwa zaidi ya asilimia 35.Vile vile, mazoezi
ya mwili husaidia kujikinga na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama
vile kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa mengine mengi.”
ameeleza Dk.Biteko
Kwa upande wa Tanzania, Dk.Biteko amesema kuwa asilimia 33 ya
Watanzania watu wazima wana uzito uliopitiliza na asilimia 28 wana
shinikizo la damu ambapo ameeleza kuwa magonjwa hayo yanachangia zaidi
ya asilimia 40 ya vifo vya mapema lakini asilimia 80 ya vifo hivyo
vinaweza kuzuilika kwa kubadili mtindo wa maisha.
Dk.Biteko ameipongeza Benki ya NBC kupitia NBC Dodoma Marathon kwa
kuunga mkono Serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya
kwani katika mwaka 2025 Marathon hiyo imelenga kuendeleza mapambano
dhidi ya Saratani ya shingo ya kizazi kwa kushirikiana na Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road.
Pia, imelenga kutoa ufadhili wa masomo ya Wakunga kupitia Taasisi ya
Benjamin Mkapa ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa
uzazi na kutoa ufadhili kwa mafunzo ya Wauguzi Maalum wa kusaidia
watoto wenye changamoto ya usonji (Autism), kwa kushirikiana na AMREF
Afrika.
Vilevile, Dk.Biteko amesema kuwa tangu NBC Dodoma Marathon
kuanzishwa mwaka 2020 imekuwa ni moja ya vilelezo vya kujenga
mshikamano, uzalendo wa kweli na kutatua matatizo mbalimbali katika
jamii ikiwemo changamoto za kiafya.
Dk.Biteko ameipongeza NBC Dodoma Marathon kwa kuendelea kuimarika
kwani mwaka 2024 ilihusisha washiriki 8,000 na mwaka huu imekuwa na
washiriki zaidi ya 12,000 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50.
Vile vile, mwaka 2024 NBC Dodoma Marathon ilikusanya kiasi cha
Sh.Milioni 300 huku mwaka 2025 ikikusanya kiasi cha Sh.
Milioni 700 sawa na ongezeko la mapato ya zaidi ya asilimia 133.33
Amesema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama NBC ambao
wameendelea kutumia mashindano ya mbio kuimarisha afya za wananchi na
kuchangia masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuokoa afya za watu.
Katika hatua nyingine, Dk.Biteko ametoa rai kwa Wizara ya Afya,
Serikali za Mitaa, Mashirika ya kiraia, Sekta binafsi na wananchi wote
kufanya mbio na mazoezi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ili kuweza
kujikinga na matatizo ya afya ambayo wananchi wanaweza kuyapata.
“Nitashukuru sana kusikia kila Taasisi imetenga kwa uchache siku moja
kwa mwezi ili kuwa na mazoezi ya pamoja, hii itasaidia kuimarisha afya
zetu na kujenga Taifa Imara. “ amesisitiza Dk.Biteko
Ameipongeza Wizara ya Afya, kwa Kampeni ya MTU NI AFYA
ambayo inawahamasisha Watanzania kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30
kila siku, kula lishe bora, kupima afya mara kwa mara na kujiepusha na
tabia hatarishi.
Kwa upande wake, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema mbio za NBC Dodoma Marathon
zimekuwa kivutio kwa wanamichezo wengi kushiriki kutokana na kundaliwa
vizuri ambapo amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kuiunga mkono benki
ya NBC katika maandalizi ya mbio hizo ambazo zimekuwa na matokeo
chanya.
Amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kuweka
mazingira mazuri ya wananchi kushiriki michezo mbalimbali pamoja na
kuendelea kujenga viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo
Arusha, Dodoma na Dar es Salama ili kuwezesha vijana kujiimarisha
kimichezo na kiafya.
Awali,Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema NBC
Marathon imekuwa ni moja ya alama za sekta binafsi katika kuwekeza
kwenye sekta ya afya na nyinginezo, akieleza kuwa katika kipindi cha
miaka mitano mbio hizo zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi
bilioni 1, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika Sekta ya Afya.
Ametaja mafanikio ya Marathon hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu na
kufanikisha kupimwa Saratani ya shingo ya kizazi kwa Wanawake zaidi ya
200,000 na kufadhili matibabu kwa wagonjwa 4,800 waliogunduliwa na
kansa hiyo katika Hospitali ya Ocean Road.
Amesema, NBC Dodoma Marathon imetoa ufadhili kwa Wakunga 100 katika
chuo cha Wakunga Morogoro kwa ushirikiano na Taasisi ya Benjamin Mkapa
Foundation huku lengo likiwa ni kufadhili wakunga 500 ifikapo 2028.
Pia ameeleza kuwa, NBC Dodoma Marathon imechangia ujenzi wa Wodi
maalum ya Wanawake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na maeneo
mengine katika maendeleo ya sekta ya afya.
Amesema msimu wa sita wa NBC Dodoma Marathon umehusisha wakimbiaji
12,000 na wamefanikiwa kukusanya shilingi milioni 700 kwa ajili ya
afya ya mama na mtoto ikilenga kuwapatia uchunguzi wa mwanzo wa
saratani ya kansa ya kizazi wanawake 10,000, kutoa ufadhili kwa
wakunga 100 na kuanzisha mpango mpya wa masomo kwa wauguzi 100
watakaoshughulika na watoto wenye changamoto ya usonji.
NBC Dodoma Marathon 2025 iliyokuwa na kaulimbiu ya Kata Wese Okoa
Maisha imehusisha wanariadha kutoka ndani na nje ya nchi ambapo
washindi wamepewa zawadi za jumla ya Sh.Milioni 80 sambamba na pikipiki 10 zilizokabidhiwa kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa hapa.