*Yawataka wadau wa kodi kutoa maoni ili mfumo ufanyiwe marekebisho
*Lengo ni kuhakikisha mfumo bora wa ukusanyaji mapato
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TUME ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini imeanza kazi rasmi na kuwataka wadau wote wa kodi kutoa maoni ya kile wanachohitaji kifanyiwe maboresho katika mfumo mzima wa ulipaji na ukusanyaji kodi.
Lengo hasa la Tume hiyo kutaka wadau kutoa maoni yao ni kuhakikisha kunakuwa na mfumo bora wa kukusanya mapato na ili kufanya tathmini kwa kushirikisha wananchi.
Sambamba na hayo,lengo jingine ni dhamira ya Serikali kufikia kiwango cha asilimia 15 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2026/27 hatua itakayoongeza uwezo wa nchi kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza kiwango cha utegemezi wa mikopo na misaada
Hayo yameelezwa leo Oktoba, 22 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue alipozungumza na Vyombo mbalimbali vya habari.
Balozi Sefue amesema wapo tayari kushirikiana na kumsikiliza kila mdau iwe mmoja mmoja, kupitia vyama vya kitaalamu, jumuiya za biashara na nyingine ili kupata maoni yatakayowasilishwa kwa Rais Dk. Samia Suluhu.
“Ikumbukwe kuwa Oktoba 4, 2024, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua rasmi Tume ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Maboresho ya Kodi.
“Kama mnavyofahamu Tume hii imeundwa kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu kero mbalimbali zinazotokana na mfumo wa kodi nchini,” ameeleza Balozi Sefue
Akizungumza kuhusu muda wa utejelezajj wa mchakato huo Balozi Sefue amesema ,Tume imepewa miezi sita lakini mchakato wa kutoa maoni utachukua miezi miwili kuanzia leo na baada ya hapo watachukua mapendekezo hayo, kuyafanyia tathmini na kuyachanganua kabla ya kuwasilisha kwa Rais.
” Tumeandaa namna bora ya kuratibu ushiriki wa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo na wananchi wanaishi nje ya nchi ikiwamo kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali.
“Tumeandaa mifumo rahisi, rafiki ya wazi ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau wa aina zote nchini ikiwemo dodoso la mtandaoni linalopatikana kupitia kiunganishi cha edodoso.gov.go.tz kwa kutumia namba ya dodoso 544978, barua pepe tume@taxreform.go.tz na maboresho. Kodi@taxreform.go.tz, namba za simu 0748 755 677, 0738 588 813” alihitimisha Balozi Sefue