NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
IDADI ya Watanzania wanaotumia bidhaa na huduma za bima imeongezeka kutoka watu milioni 5.6 mwaka 2021 hadi milioni 26.8 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko kubwa linaloashiria kukua kwa uelewa na matumizi ya huduma za bima nchini.
Hata hivyo idadi hii inatarajia kuongeza zaidi na kufikia watu Milioni 40 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, mchango wa sekta ya bima katika Pato la Taifa (GDP) umeongezeka kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi asilimia 2.11 mwaka 2025, huku kiwango cha wananchi wanaotumia na kunufaika na huduma za bima kikiongezeka kutoka asilimia 8.9 hadi asilimia 39.3 katika kipindi hicho.
Sambamba na hayo thamani ya ada za bima zilizoandikishwa imeongezeka kutoka Sh.Bilioni 911 mwaka 2021 hadi Sh.Trilioni 2.55 mwaka 2025, huku madai ya bima yaliyolipwa yakiongezeka kutoka Sh.Bilioni 397.57 hadi Sh. Trilioni 1.29.
Pia,mali zilizowekezwa na kampuni za bima zimeongezeka kutoka Sh. Bilioni 939.69 hadi Sh.Trilioni 2.24, hali inayoonesha kuimarika kwa uwezo wa sekta hiyo kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Bima, Dk Baghayo Saqware leo Jumatatu Novemba 16,2025 wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amebainisha kuwa ongezeko hilo limechangiwa na usimamizi madhubuti wa sekta ya bima pamoja na jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma hizo.
Kamishna Dk.Saqware amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeongeza uwezo wake wa kitaasisi, ambapo mali za mamlaka hiyo zimeongezeka kutoka Sh.Bilioni 11.18 mwaka 2021 hadi Sh.imBilioni 21.72 mwaka 2025.
Amesema idadi ya watoa huduma za bima pia imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 10,940 mwaka 2025, huku ajira rasmi katika sekta hiyo zikiongezeka kutoka 3,737 hadi 15,398.
Kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, Dk.Saqware amesema Serikali imeendelea kupanua wigo wa huduma hizo kupitia awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango huo, iliyozinduliwa Oktoba 22, 2026 na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
Amesema katika awamu ya kwanza kaya 198,709 za wananchi wasio na uwezo zilihakikiwa na kupatiwa kadi za bima ya afya, huku awamu ya pili ikilenga kusajili kaya nyingine 625,000 pamoja na kuwawezesha wananchi wenye uwezo wa kuchangia kujiunga na mfumo huo.
Wakati huo huo,Dk.Saqware anetumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi ambao bado hawajajiunga na bima ya afya kufanya hivyo kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kampuni binafsi zilizosajiliwa na kuidhinishwa na TIRA, akisisitiza kuwa bima ya afya ni kinga ya kifedha inayomsaidia mwananchi kupata matibabu bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama.
Amesema TIRA itaendelea kusimamia kampuni za bima kuhakikisha zinazingatia sheria na kanuni, zinalipa madai ya wateja kwa wakati na zinakuwa na mitaji pamoja na uwezo wa kifedha unaokidhi matakwa ya kisheria.
Katika hatua nyingine Kamishna huyo wa Bima nchini ameeleza kuwa mamlaka hiyo pia imeimarisha mifumo ya kidijitali, elimu ya bima kwa umma, utatuzi wa migogoro na udhibiti wa udanganyifu ili kulinda haki na maslahi ya watumiaji wa huduma za bima nchini.
Amesisitiza kuwa lengo la TIRA ni kuhakikisha sekta ya bima inakuwa imara, endelevu na yenye ushindani wa haki, huku ikichangia ustahimilivu wa uchumi na kulinda wananchi dhidi ya vihatarishi mbalimbali.

