NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetumia mashindano ya ngumi kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme, sambamba na kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini.
Katika kuunga mkono wanamichezo wanaolitangaza Taifa, TANESCO imemzawadia bondia Kalolo Amiri Sh milioni mbili pamoja na jiko la kisasa la umeme (Smart Pika), baada ya kuibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake Kurta Pabular kutoka Ufilipino.
Akikabidhi zawadi hizo, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Wadau wa TANESCO, Augustino Kasale, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo na kutambua mchango wa wanamichezo wanaoliwakilisha Taifa katika mashindano mbalimbali.
Amesema jiko hilo linatumia umeme kwa ufanisi, hivyo zawadi hiyo pia inalenga kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati hiyo nchini.
“TANESCO inaendelea kuunga mkono michezo nchini. Tumetoa zawadi hizi kwa sababu tunatambua mchango wa wanamichezo wanaolitangaza Taifa letu. Pia tunaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia umeme kupikia,” amesema Kasale.
Kwa upande wake, bondia Kalolo Amiri ameishukuru TANESCO kwa kuunga mkono mchezo wa ngumi, akisema zawadi hizo zimeongeza ari na motisha ya kuendelea kufanya vizuri katika mashindano yajayo.
“Namshukuru sana Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kwa kuona umuhimu wa kutambua mchango wetu katika michezo. Hatua hii imetupa nguvu zaidi ya kujituma na kujiandaa vizuri kwa mapambano yajayo, hususan yale yanayohusisha kuiwakilisha nchi yetu,” amesema Kalolo.
Katika pambano hilo, Kalolo aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya Pabular kutoka Ufilipino baada ya kumalizika kwa raundi nane, katika mashindano yaliyohusisha mapambano mbalimbali ya ngumi.
Mgeni rasmi katika mashindano hayo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Mahmoud Thabit Kombo.





