NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WANAFUNZI wa Klabu ya Vipimo (Vipimo Club) kutoka Shule ya Msingi Mtemi Mazengo ya jijini Dodoma, wamegeuka walimu kwa siku moja baada ya kumpa elimu ya vipimo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,Dennis Londo, katika banda la Wakala waVipimo (WMA), kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane, Dodoma.
Agosti 7, 2026, Naibu Waziri Londo alishangazwa na ufasaha wa wanafunzi hao walipomweleza umuhimu wa vipimo sahihi, kuandika kwa usahihi vifungashio katika bidhaa zilizofungashwa pamoja na madhara ya lumbesa.
“Nimefurahishwa sana. Watoto hawa ni mabalozi wazuri wa jamii. Uwekezaji wa WMA katika kizazi kijacho unaleta matokeo,” alisema.
Wanafunzi hao walikuwa katika ziara iliyoratibiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni sehemu ya mpango wa elimu ya vipimo kwa vitendo.



