NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, amewahimiza Watanzania kutembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kujionea mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya nishati nchini.
Akizungumza katika viwanja vya Sabasaba, Kingu amesema maonesho ya mwaka huu yana umuhimu wa kipekee kwani yanaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1976, hatua inayodhihirisha mchango mkubwa wa maonesho hayo katika kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya taifa.
“Nawaomba Watanzania wafike viwanja vya Sabasaba na kutembelea banda la Wakala wa Nishati Vijijini ili wajifunze na kujionea kazi mbalimbali zinazotekelezwa na wakala wetu katika kuwahudumia wananchi,” amesema Kingu.
Amesema REA imeendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wote, hususan wanaoishi vijijini na maeneo ya pembezoni mwa nchi.
Kwa mujibu wa Kingu, hadi sasa REA imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 12,318 nchini kote kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakandarasi wa ndani pamoja na wa nje.
Aidha, amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha umeme unafikishwa katika mitaa na vitongoji vyote nchini, ambapo kati ya vitongoji 68,359 vilivyopo Tanzania, zaidi ya 40,000 tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme.
“Hii ni hatua kubwa inayostahili kupongezwa na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya nishati vijijini. Tunatarajia ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini vitakuwa vimefikiwa na umeme,” amesema.
Ameeleza kuwa umeme si huduma ya kuwasha taa pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Kingu, upatikanaji wa umeme umechangia kuboresha huduma katika shule, vituo vya afya na zahanati, sambamba na kuwezesha wananchi kupata maji safi na salama kupitia matumizi ya pampu za maji zinazotumia umeme.
“Zamani pampu nyingi za maji zilikuwa zinatumia mafuta na majenereta, jambo lililokuwa na gharama kubwa. Sasa umeme umeleta suluhisho endelevu kwa wananchi wa vijijini, hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma bora za maji,” amesema Kingu.
REA ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, yakibeba kaulimbiu ya kuhamasisha biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi wa taifa.

