NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amepiga marufuku kwa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuwaambia wafanyabiashara kuwa hawana vigezo vya kufanya biashara, akisisitiza kuwa jukumu lao ni kuwasaidia kufikia vigezo hivyo ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Kapinga ameyasema hayo Mei 9,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa wadau kuhusu kutumia fursa ya kuuza bidhaa katika soko la China bila ushuru (Zero Tariff) ulioandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Jamhuri ya Watu wa China- Tanzania.
Waziri huyo amesema serikali imeamua kuhamia katika mfumo wa uwezeshaji badala ya udhibiti, akieleza kuwa taasisi za umma zinapaswa kuwa sehemu ya suluhisho kwa wafanyabiashara badala ya kuwa kikwazo katika safari yao ya kibiashara.
Amesema katika kipindi hiki cha ushindani wa kimataifa, taasisi za serikali zinapaswa kuboresha mifumo yao ya utoaji huduma na kuhakikisha wafanyabiashara wanapata mwongozo, taarifa na msaada wa haraka ili waweze kufikia masoko ya nje, hususan soko la China.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ametangaza kuwa serikali itaanzisha dawati maalum la kuwahudumia wauzaji bidhaa wanaolenga soko la China, likiwa na wataalamu wenye uwezo wa kuzungumza lugha ya Kichina ili kusaidia kurahisisha mawasiliano na kufungua zaidi fursa za biashara.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la China, ambalo ni miongoni mwa washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania.
Aidha, amezitaka taasisi za serikali kuharakisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kushughulikia maombi ya wafanyabiashara ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na kuongeza uwazi pamoja na ufanisi.
Amezitaja taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuwa zimeanza kufanya vizuri katika maboresho ya mifumo yao, huku akiitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuongeza kasi ya utekelezaji.
Pia amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza katika ubora wa bidhaa, kuongeza thamani, usindikaji na ubunifu ili kujenga ushindani mkubwa katika soko la China na masoko mengine ya kimataifa.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha fursa za biashara za kimataifa zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya uchumi wa taifa, ajira na maendeleo ya viwanda.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema sera ya ushuru sifuri kwa bidhaa za Tanzania kwenda China itasaidia kuongeza ushindani wa bidhaa katika masoko, huku akibainisha kuwa mauzo ya Tanzania kwenda China yamejikita zaidi katika bidhaa za kilimo zenye ushindani.
Amefafanua kuwa mwaka 2025, kiwango cha biashara kati ya China na Tanzania kilifikia dola za Marekani milioni 11.2, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia kuvuka kiwango cha milioni 10.
Ameongeza kuwa kupitia sera hiyo, bidhaa za Tanzania kama ufuta na korosho zinatarajiwa kunufaika zaidi, huku bidhaa kama dhahabu na vito vya thamani zitaendelea kuongeza mchango wake katika mauzo ya nje kutokana na ushindani wa bei katika soko la China.



