NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
ZAIDI ya mataifa 50 yanatarajiwa kushiriki Mkutano wa 30 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Vyuo vya Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Duniani (IAPTC) utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu nchini Tanzania, ukiwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha na kuleta ubunifu katika operesheni za ulinzi wa amani duniani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN).
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati akifungua kikao cha maandalizi ya mkutano huo cha Kamati Tendaji ya IAPTC,Mei 6,2026 Mwenyekiti wa kikao hicho kutoka Italia, Brigedia Jenerali Andrea Paris amesema kwa kawaida mkutano huo hukutanisha kati ya mataifa 50 hadi 60, huku jumuiya hiyo kwa ujumla ikiwa na wanachama kutoka takriban mataifa 90 duniani.
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kutathmini kazi za mwaka mzima za chama hicho na kubaini njia mpya za kuimarisha operesheni za ulinzi wa amani ili ziweze kuwa na ufanisi zaidi katika dunia yenye changamoto nyingi za kiusalama.
Kuhusu changamoto zinazozikabili baadhi ya vituo vya mafunzo ya ulinzi wa amani, ikiwemo uhaba wa rasilimali watu na vifaa, Brigedia Jenerali Paris amesema vituo hivyo vinaendelea kushirikiana kwa kubadilishana wataalamu, uzoefu na mawazo hata nje ya mikutano rasmi, kwa lengo la kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya operesheni.
Amefafanua kuwa vituo vya mafunzo ya ulinzi wa amani vina nafasi muhimu katika dunia ya sasa, kwani vina jukumu la kuwajengea uwezo walinda amani ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kuleta utulivu na amani duniani.
Aidha, amesema katika kipindi cha miaka 30 ya uwepo wa IAPTC, mafanikio makubwa yamepatikana katika kuleta ubunifu kwenye operesheni za ulinzi wa amani, kuibua mawazo mapya kwa mashirika ya kimataifa pamoja na kuweka viwango vya pamoja vya utendaji kwa wanajeshi, polisi na raia wanaoshiriki katika operesheni hizo.
Akizungumzia sababu za kuchagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu, amesema nchi hiyo imebarikiwa kwa mazingira mazuri na ina sifa zote zinazostahili kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu wa kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa 30 na kwamba fursa hiyo haijaja kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya mchango mkubwa wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani duniani.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Brigedia Jenerali Itang’ar amesema mchango wa Tanzania katika agenda ya amani na usalama duniani unatambulika kimataifa, jambo ambalo limeifanya nchi kupewa heshima ya kuandaa mkutano huo muhimu unaotarajiwa kuwakutanisha wadau wa ulinzi wa amani kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema kuwa kupitia TPTC, Tanzania imekuwa ikichukua hatua za kuonyesha dhamira yake ya kuunga mkono juhudi za kimataifa za kuleta amani, na ndio msingi uliowezesha nchi kupewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria.
Kuhusu mchango wa Tanzania katika kusaidia mataifa ya Afrika yanayokumbwa na migogoro, amesema jukumu la usalama wa taifa hubaki kuwa la nchi husika, lakini kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Tanzania itaendelea kuwa tayari kutoa mchango wake pale itakapohitajika katika juhudi za kurejesha amani.
Hata hivyo amesema kuwa mafanikio ya mkutano huo hayatapatikana bila ushirikiano wa wajumbe na wanachama wa kamati hiyo, akitoa wito kwa kila mshiriki kuchangia uzoefu na nguvu zake ili kuhakikisha mkutano wa Novemba unakuwa wa mafanikio makubwa
Aidha, amesisitiza kuwa jukumu la vituo vya mafunzo ya ulinzi wa amani ni muhimu katika kuandaa wataalamu na vikosi vya kulinda amani, ili kuhakikisha operesheni za kimataifa za amani zinafanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa.





