NA MWANDISHI WETU,MBOZI,SONGWE
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewahakikishia wakulima wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe na kuwa mbolea zote za kupandia, kukuzia na kubebeshea kwa msimu wa kilimo zinapatikana kwa wingi na kwa wakati.
Mamlaka imefanya ufuatiliaji maalum Wilaya ya Mbozi ili kubaini hali halisi ya upatikanaji na matumizi ya mbolea. Ufuatiliaji huo umebaini kuwepo kwa zaidi ya tani 3,544 za mbolea mbalimbali zinazouzwa katika maduka ya wafanyabiashara waliothibitishwa.
Aidha, mamlaka ilitembelea mashamba ya wakulima waliolalamikia matumizi ya mbolea aina ya DAP ili kuchunguza hali ya mazao shambani pamoja na kubaini kama manunuzi ya mbolea hiyo yalifanyika kupitia mfumo rasmi wa ruzuku.
Katika zoezi hilo, TFRA ilitoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, ikiwemo umuhimu wa kununua mbolea kupitia mfumo wa ruzuku kwa kutumia namba za mkulima, pamoja na kuchagua mbolea sahihi kulingana na hatua ya ukuaji wa zao, hususan kwa mazao yaliyokuwa tayari yanaingia hatua ya kuweka mbolea ya kukuzia.
Mafunzo hayo yalitolewa kwa wakulima 541 wa Kata za Mahenje, Halungu, Magamba na Itaka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, ambapo wakulima hao wamepatiwa elimu juu ya umuhimu wa kupima afya ya udongo kabla ya matumizi ya mbolea.
Elimu hiyo inalenga kumuwezesha mkulima kutambua virutubisho vilivyopo na vinavyokosekana kwenye udongo wake, hatua inayosaidia kuchagua mbolea inayofaa na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo,Ofisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Chrysanthus Funda, amesema kupima sampuli ya udongo humsaidia mkulima kuchagua mbolea sahihi kulingana na mahitaji ya udongo wake, hivyo kuepusha matumizi ya mbolea isiyofaa ambayo husababisha mbolea kuonekana kutofanya kazi ipasavyo.
Amefafanua kuwa mara nyingi changamoto ya mbolea kudaiwa kutokuwa na ubora hutokana na kutotumika kwa mbolea inayolingana na mahitaji ya udongo husika.
Kwa upande wake,Ofisa Udhibiti Ubora wa TFRA, Mushoborozi Christian, amewahimiza wakulima kuhakikisha wanasajili naÿ kuhuisha taarifa zao katika mfumo wa ruzuku ya mbolea, akieleza kuwa usajili huo ni msingi wa mkulima kupata pembejeo kwa wakati, kwa bei nafuu na zenye ubora unaothibitishwa na Serikali.
Ameongeza kuwa kununua mbolea nje ya mfumo rasmi huwaweka wakulima katika hatari ya kupata mbolea isiyokidhi viwango, hali inayosababisha hasara na kushuka kwa uzalishaji.
Mushoborozi amebainisha kuwa TFRA imeendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji wa mbolea nje ya mfumo rasmi, ikiwemo kufutiwa leseni, huku akiwataka wakulima kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo hivyo.
Naye Yohana Kibona, mkulima kutoka Kijiji cha Halungu, ameishukuru TFRA kwa mafunzo hayo, akisema yameongeza uelewa wa wakulima kuhusu mbolea bora na umuhimu wa kununua pembejeo kupitia mfumo rasmi wa ruzuku.






