NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMANDA wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema kuwa afya ya akili na uimara wa kisaikolojia ni nguzo muhimu katika operesheni za ulinzi wa amani, hasa katika mazingira ya sasa yenye changamoto nyingi na misukosuko ya kiutendaji.
Brigedia Jenerali Itang’are ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Mafunzo ya Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia (MHPSS) kwa watendaji wa Umoja wa Mataifa, Awamu ya 02/25.
Amesema kuwa Umoja wa Mataifa unatambua kwa kiwango kikubwa umuhimu wa afya ya akili kama uti wa mgongo wa utayari wa kiutendaji, mafanikio ya misheni na kulinda utu wa binadamu.
“Elimu ya afya ya akili na uimara wa kisaikolojia kwa walinzi wa amani ni muhimu na ndio maana Umoja wa Mataifa unatambua jambo hilo kama uti wa mgongo wa utayari walinzi kiutendaji na mafanikio katika misheni ya ulinzi wa amani,” amesema
Hata hivyo amesisitiza kuwa ujuzi na maarifa waliyopata wahitimu hai haupaswi kubaki katika nadharia pekee, bali yanapaswa kutumika kwa vitendo katika majukumu yao ya kila siku.
Aliwahimiza wahitimu kuwa mabalozi wa ustawi wa kisaikolojia katika vikosi vyao na kuwasaidia wenzao wanaoweza kukumbana na changamoto za kiakili au kihisia katika maeneo ya operesheni.
Hata hivyo Brigedia Jenerali Itang’are aliwapongeza washiriki wote kwa kujituma, nidhamu na ushiriki wao wa kina katika kipindi chote cha mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya United Nations Institute for Training and Research (UNITAR).
Amesema takribani washiriki 48 wamehitimu mafunzo hayo ambapo kwa kozi ya MHPSS washiriki 19 wameshiriki mafunzo hayo na kwa kozi ya Logistics walikuwa washiriki 29.
“Maofisa hawa walipata mafunzo mazuri ambayo yatawawezesha kuingia katika mifumo ya utendaji katika Idara ya logistics katika umoja wa Mataifa na vilevile itawawezesha kufanya kazi katika misheni nyingine,”amesema
Aliwasisitizia washiriki kudumisha viwango vya juu vya weledi, huruma na uadilifu wanapotekeleza kanuni za MHPSS katika majukumu yao.
Akihitimisha, alionesha imani kuwa Awamu ya 02/25 itatoa mchango mkubwa katika kuboresha ustawi, uimara na utendaji wa walinda amani wanaohudumu katika maeneo mbalimbali duniani.




