NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amefunguka mambo mazito zaidi ya kumi wakati akizungumza na Watanzania kupitia Baraza la Wazee wa Jiji la Dar es Salaam.
Katika mkutano huo uliojaa utulivu na usikivu mkubwa umefanyika leo Desemba 2, 2025 jijini Dar es Salaam na kukutanisha wazee mbalimbali kutoka sehemu tofauti tofauti za jiji pamoja na viongozi wakiwemo mawaziri, manaibu Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Wakuu wa Wilaya.
Akizungumza na Baraza hilo la Wazee wa Jiji la Dar es Salaam, Rais Samia amezungumza kwa uwazi, uthabiti na msisitizo kuhusu masuala ya msingi yanayohusu amani ya nchi, mustakabali wa uchumi, mahusiano ya kimataifa na umoja wa kitaifa.
Mbele ya Baraza la Wazee wa Dar es Salaam, Rais Samia aliweka hadharani hoja kadhaa nzito, akitoa taswira mpya ya namna serikali inavyokabiliana na changamoto za sasa na kuweka mwelekeo wa miaka ijayo huku akisisitiza juu ya amani na utulivu katika nchi.
Akianza na hoja ya kile kilichotokea Oktoba 29, 2025 amesema kuwa yaliyotokea siku hiyo hayakuwa maandamano bali ni vurugu na machafuko yaliyoandaliwa kwa madhumuni ya kuiangusha Serikali hivyo nguvu iliyotumika kuyadhibiti inaendana na tukio husika.
Amesema vurugu hizo zilizotokea zilikuwa na nia ovu na kwamba vijana wengi walihusishwa kwa kufuata mkumbo bila kuelewa madhara yatakayotokea hivyo Serikali ililazimika kuchukua hatua za haraka kwa lengo la kulinda usalama wa nchi na raia wake.
“Vurugu zilizotokea Oktoba 29 na kuendelea 30 si desturi wala utamaduni wetu, kila mtanzania aliyeumia na kupoteza maisha ni mtu wetu mwenye haki saw ana wengine. Haki ya kuishi na kuwa huru ni tunu zetu watanzania wote kwa hiyo hakuna sababu ya watanzania kuumizana na kunyimana uhuru. Inatia uchungu kuona wachache walioratibu fujo zile wakitaka kuwafanya wenzao wawe kafara kwa malengo yao ya kisiasa yaliyojaa ubinafsi tofauti na siasa iliyopo,” amesema
Amesema takwimu zinatolewa sasa hivi, kuna majengo kadhaa ya Serikali yameunguzwa, miradi kadhaa iliyojengwa kwa maslahi ya Wananchi imeunguzwa, Vituo vya mafuta, biashara binafsi za watu, magari ya Serikali pamoja na vituo vya polisi.
“Sasa nataka tuwe na jina la hayo ni maandamano au vurugu? maandamano tuliyoyazoea na kuyakubali ndani ya Katiba ni yale Watu wameudhika na kitu tunaomba tuandamane tueleze tutatoka point moja hadi Mnazimmoja au popote pengine na mabango yanaeleza maudhi yetu na Polisi wanawasindikiza vizuri hadi wanapofika” amesema Rais Samia na kuongeza
“Kuunguza miradi ya Serikali, vituo vya Polisi na kwenye kituo cha Polisi unakwenda kufanya nini? ni kwenda kuvamia na wapate silaha, madhumuni ya kuwa na silaha mkononi ni nini? haya hayakuwa maandamano zilikuwa vurugu zilizoandaliwa kwa madhumuni maalum” amesema
Amesema kuwa serikali inawajibu na kwamba wanaapa kuilinda mipaka ya nchi, Raia na mali zao, hivyo katika hali hiyo nguvu iliyotumika iliendana na tukio lililopo, na kuhoji kwamba wanapoambiwa walitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile… nguvu ndogo ilikuwa ni ipi?.
“Ilikuwa tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe? hapo patakuwa pana Dola kweli? Dola haipo hivyo, sio Tanzania tu hata mataifa mengine watu wakiandamana wanaweka nguvu kubwa, sasa wanapokuja kutulamu mlitumia nguvu kubwa wao walitaka nini?, tujiulize je hawa ndio wafadhali wa kile kilichofanyika?.
“Walitaka tuangalie ile mambo hadi ifanikiwe walichowapa fedha, walichowatuma? hapana” tuliapa kulinda nchi hii na mipaka yake, usalama wa raia na mali zao kwahiyo kama wanavyofanya wao na sisi tutafanya vilevile kuilindi nchi yetu” , amesema Rais Samia
Hata hivyo Rais Samia alisisitiza kuwa haitakiwi kuruhusu mkoa wa Dar es Salaam uchafuliwe kwani ndio taswira nzima ya Tanzania duniani huku akibainnisha kuewa asilimia 10 ya watanzania wanaishi katika mkoa huo hivyo vurugu zinapotokea huathiri nchi nzima.
“Tutasimama na kuilinda nchi hii kwa nguvu zote, nasema yaliyopita si ndwele tugange yajayo, kama madai ya wenzetu ni Katiba hakuna aliyekataa kurekebisha Katiba ya nchi hii, Mnakumbuka niliunda Tume ya haki jinai ikaenda na kuniletea haya ndio wanayoyaona watanzania, katika kuyatekeleza kuna ya muda mfupi, wa kati na mrefu.
“Ya muda mfupi na kati mengi tumeyatekeleza, lililobaki ya muda mrefu ni ya Katiba ambalo nimesema tutalitekeleza na mkisoma ilani ya uchaguzi ya CCM nilisema ndani ya siku 100 nitaunda tume itakayofanya maridhiano kisha tuingie katika Katiba, sasa mnaendaje kwenye Katiba wakati huku nyuma mpo vipande vipande,” amesema Rais Samia.
Kuhusu vijana
Rais Samia amesema Vijana wengi wa Tanzania hawana uzalendo na hilo Serikali imeliona hivyo italifanyia kazi huku akisisitiza kuwa kundi hilo halikuandamana kwa sababu ya ugumu wa maisha bali ni kwakuwa walilipwa na wengine walifuata mkumbo.
“Vijana wetu wameingizwa barabarani wakaimbishwa wimbo wasioujua kwamba yaliyokea Madagasca yatokee hapa, wanadai haki, haki gani!?, mvute Kijana pembeni muulize unadai haki gani!?, na hiyo haki hawakuweza kuidai kwa njia gani hadi waingie barabarani wafanye vurugu?, walipwe wakachome vituo?,
“Jingine wanalobebeshwa wameingia njiani eti kwa ugumu wa maisha, Astaghfrullah, ningekuwa na uwezo ningewabeba Vijana wa Tanzania nikawatupe kwenye nchi kadhaa za Afrika pamoja na majirani zetu wakaone ugumu wa maisha uliokuwepo, halafu waseme kwamba kwao Tanzania ni pahala pema” amesema na kuongeza
“Mwenye ugumu wa maisha kwa raha zake kabisa kweli ataingia njiani akaimbe woyoo woyoo huo ugumu wa maisha?, wenye ugumu wa maisha ataingia kupambana kutafuta chakula, hawa hawakuwa na ugumu wa maisha walikuwa na sababu zao nyingine, Watafiti wafanye utafiti waangalie nafasi ya Tanzania kwenye ugumu wa maisha” amesema
Rais Samia amesema kuwa vijana nchini wasimezeshwe tu na wenyewe wakameza hapana, haya yametokea na kuwajuza kuwa kundi hilo la vijana limekuwa tu bila elimu ya uzalendo.
“Vijana wazalendo hata upinzani hawakukubaliani na lile, walikuja kutuambia kaeni vizuri wanapanga kufanya hivi, vijana wetu wengi Tanzania sio wazalendo na hilo Serikali tumejifunza na tutakwenda kulifanyia kazi” amesema Rais Samia
Amesema baada ya kuiona hilo ndio maana ameunda Wizara nzima ya Vijana ili kushughulikia Vijana kwa upana, hivyo akisisitiza kuwa vijana hawakuwa na sababu ya msingi ya kuingia barabarani isipokuwa kutumwa na kuingilia mambo yasiyowahusu.
Kuhusu TEC
Hata hivyo Rais Samia amewataka viongozi wa dini kuacha kuvuruga amani na kujivisha majoho ya kutoa matamko kwa niaba ya Watanzania wote huku akisema ndani ya muda wake madarakani Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) limetoa matamko manane ingawa wapo baadhi ya viongozi wa TEC wameyapinga matamko hayo.
Akiongea na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Samia amesema inapaswa kuangalia taasisi za Dini ambazo nazo kwa namna moja ama nyingine wamejiingiza kwenye mkumbo huo.
“Unajua ukiwa Kiongozi lazima ukubali wakati fulani kukosa umaarufu lazima ukubali, Taasisi zetu za Dini, tunasema Tanzania haina dini ila Watanzania tuna dini, kikatiba na sheria ya nchi hakuna dhehebu limepewa mamlaka ya kutoa matamko kwa niaba ya wengine”
“Viongozi wa dini msijivishe majoho ya kwamba nyinyi mtaweza kuover-run nchi hii hakuna, tutakwenda kwa Katiba ya nchi hii, hatutoendeshwa na madhehebu yoyote ya dini, madhehebu ya dini na wafuasi wao, ubora wa dini upo mioyoni kwetu, wale wanaowaamini ndio wanajua ubora wa dini yao, hakuna over-riding hapa kwamba Mimi dini yangu ndio itaover-ride wengine na hata nikilitoa tamko langu ndio kubwa hata wenyewe wanatofautiana” amesema
Amesema yeye toka amekaa matamko manane yametolewa na TEC lakini ukienda chinichini wenyewe kwa wenyewe wanapingana matamko yale hayafanyi kazi vizuri.
“Wenyewe wanapingana kwasababu waliosimama kwenye mstari wa haki wanaona ile ni batili iliyofanyika, Tanzania ni nchi ya umoja na mshikamano, amani na utulivu ndio ngao zetu tusivurugwe ndugu zanqu” amesema Rais Samia na kuongeza
“Amani na utulivu ndio ngao yetu tusiivurugwe, kama mtu umpendi anayeongoza tuvumilie tu ataondoka wakati wake ukifika, Kama umpendi Samia sijui kwa sababu ya dini yake au anapotoka, vumilia na subiri ataondoka muda wake ukifika,” amesema
Kuhusu vyama vya upinzani
Rais Samia maesema hajakizuia chama chochote cha upinzani kuingia katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu na kwamba kama kuna haki yoyote chama cha upinzani kinadai wanakaribishwa katika meza ya mazungumzo na si kuanzisha vurugu.
“Hatujawazuia wao kuingia katika uchaguzi na kama kuna haki yeyote inadaiwa hakuna siku nyingine mpaka siku ya uchaguzi, katika hili tunaambiwa kuna waratibu wanaoishi nje ya nchi tunawajua wengine ambao ni watanzania tunajua ni shida za maisha walizonazo wanafanya hao kisha wanalipwa hivyo wamekosa uzalendo,” amesema Rais Samia
Amesisitiza kuwa wapinzani waliishiwa nguvu kwa lugha ya vijana waliishiwa paw ana kwamba katika vyama vyao hawapo sawa hivyo wasihirahumu serikali kwa sababu hawakudhuiriwa kuingia katika uchaguzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Matimbwa amesema Mwenyekiti wa Baraza la Wazee amesema kuwa wanampongeza Rais Samia kuchukua hatua ya kuunda Tume ya uchunguzi ili kuweza kubaini kilichotokea Oktoba 29, mwaka huu wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Amesema licha ya maagizo hayo pia Rais aliamuru kuachiwa kwa vijana waliofuata mkumbo na kuingia katika maandamano bila kujua na kwamba wanafarijika amri hiyo imefuatwa na tayari vijana wengi wameachiwa na kurejea kwenye familia zao.
Matimbwa amessitiza kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa kisiwa cha amani hivyo wazee hawana mashaka kwamba chini ya Rais Samia Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani.
“Pia tumefarijika kuona Wizara ya Vijana imeundwa tunaimani kupitia Wizara hii matatizo mengi ya Vijana yatasikilizwa na kuchukuliwa hatua, tunamshukuru Rais kwa kutupatia ahadi kwamba wazee sasa wayapata bima ya afya katika siku 100 za uongozi wake, bima hiyo ni faraja kubwa kwa kundi hili ambalo wengi wao wamekuwa wakisumbuliwa na maradhi mbalimbali,” amesema
Hata hivyo Matimwa amesema wazee wa Dar es Salaam, wanatambua kuwa kampeni zilikwenda vizuri kwa vyama vyote na michakato yote ilifanyika kwa amani na utulivu na kwamba upigaji kura ulikwenda vizuri hadi pale fujo na vurugu zilizopotokea.












