NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Tanzania inakusudia kuwa miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika kwa kuvutia uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara, hatua inayotekelezwa kupitia Dira 2050 na mashirika ya uwekezaji kama TISEZA.
Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji pamoja na uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Watoa Huduma kwa Wawekezaji, Waziri amesema Dira 2050 inalenga kubadilisha sekta ya umma kutoka kuwa mdhibiti kwenda kuwa mwezeshaji wa biashara na uwekezaji, huku ikibaini malengo makuu matano yanayojumuisha urahisi wa kufanya biashara, uwepo wa mifumo imara ya kidijitali, na jamii inayozingatia uwekezaji na akiba.
Profesa Mkumbo amesema TISEZA, iliyoundwa kutokana na kuunganishwa kwa TIC na EPZA, itakuwa chombo kikuu cha kuratibu, kuhimiza na kuendeleza uwekezaji nchini amesisitiza kuwa taasisi hiyo ndiyo “mtafsiri wa ndoto ya Taifa” na kazi yake ni kuhakikisha maono ya Dira 2050 yanakuwa matokeo halisi.
Aidha, Waziri huyo amesema kuwa TIC ilisajili miradi 2,792 kati ya mwaka 2021–2025 yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 33.2 na kuunda ajira takribani 758,900, jambo linalotoa msingi imara kwa TISEZA kuendeleza na kuongeza uwekezaji hata hivyo, amesema Tanzania bado haijafikia lengo la kuwa miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika.
Aidha vigezo muhimu vya kuvutia wawekezaji vilivyotajwa na Waziri Mkumbo ni pamoja na uthabiti wa kisiasa, utawala bora, urahisi wa kufanya biashara, upatikanaji wa mitaji, ukubwa wa soko, na fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta kama kilimo, viwanda, madini na nishati.
Profesa Mkumbo amesema Serikali inakamilisha MKUMBI II, mkakati utakaondoa vikwazo vya uwekezaji na kuimarisha urahisi wa kufanya biashara, huku Bodi ya TISEZA ikipewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa vigezo hivi kwa kuzingatia malengo ya Dira 2050.
Aidha, Wizara ina mpango wa kuwainua vijana kupitia Kituo Maalum cha Wawekezaji Vijana (Youth Investors Resource Centre), kitakachotoa mafunzo, uwezeshaji wa viwanda, ardhi, na uunganishaji na taasisi za kifedha. Mpango huu unalenga kuhimiza ujio wa vijana katika sekta ya viwanda nchini kote.
Profesa Mkumbo amesema TISEZA pia itasogeza huduma za uwekezaji hadi mikoa yote ifikapo mwaka 2028, kuanzisha miundombinu ya viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi, na kuendeleza vivutio vipya vya kiuwekezaji.
Aidha, amebainisha kuwa kutakuwa na jukwaa rasmi la kukutana na wawekezaji kila robo mwaka kuanzia Januari 2026, kusikiliza changamoto, kupokea mapendekezo na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Pia amezungumzia mpango wa kipekee wa Bagamoyo na miundombinu ya kiuwekezaji itakayovutia viwanda vitakavyouza bidhaa ndani na nje ya nchi ni hatua muhimu ya kushirikiana na sekta binafsi ya ndani na nje kuhakikisha ujenzi wa bandari na shehena za mizigo unakamilika ipasavyo.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara ,Judith Kapinga, amesema anashukuru jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza uwekezaji wa kiuchumi nchini. Amesisitiza kuwa TISEZA itasimamia vipimo, ushindani wa soko na maendeleo endelevu ya uwekezaji, huku akihakikisha malengo ya Dira 2050 yatafikiwa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na wadau wengine.
Naye Mkurugenzi mkuu wa TISEZA,Gilead Teri, amesema taasisi yake imeandaa mipango ya kutoa huduma mahala pamoja kwa wawekezaji ili kuhakikisha kuwa baada ya kupata leseni, wawekezaji wanapata suluhisho la haraka kwa changamoto zao zote, jambo linalofanya uwekezaji nchini kuwa rahisi na wa kuvutia.
Profesa Mkumbo amesema Tanzania bado ni nchi salama kwa uwekezaji, huku changamoto za hivi karibuni zikionyesha nafasi ya taifa kuimarisha umoja, amani, na fursa za kiuchumi kwa wananchi wake.
Waziri amehitimisha kwa kutoa malengo ya TISEZA kwa mwaka wa fedha 2025/26: kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni 15 na kusajili miradi angalau 1,500 katika sekta zote za uwekezaji nchini.









