FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameitaka Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) kuongeza ubunifu na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato, akisema teknolojia zinazozalishwa na wataalamu wa taasisi hiyo zina uwezo wa kuvutia uwekezaji binafsi, kukuza bunifu na kuongeza ajira, hivyo kupunguza utegemezi wa serikali katika kuendeleza sekta ya viwanda.
Waziri Kapinga ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi katika taasisi hiyo, akibainisha kuwa TIRDO inapaswa kuimarisha uwezo wake wa kutengeneza teknolojia zinazotumika moja kwa moja katika viwanda na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
Waziri Kapinga ameeleza kuwa TIRDO ina nafasi muhimu katika kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani, hivyo kunahitajika mkakati wa kuimarisha tafiti na matumizi ya teknolojia za kisasa zinazojibu changamoto za uzalishaj amesisitiza kuwa ushirikiano na sekta binafsi ni muhimu ili kuongeza matumizi ya bunifu zinazotengenezwa na wataalamu wa ndani.
Amesema tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo zinapaswa kutafsiriwa katika matumizi halisi viwandani, ili kupunguza gharama kwa wazalishaji na kuongeza ufanisi wa uzalishaji ameongeza kuwa malengo ya nchi ya kujenga uchumi wa viwanda hayawezi kufikiwa bila taasisi kama TIRDO kufanya kazi kwa ufanisi na ubunifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TIRDO, Mhandisi Bashiri Mrindoko, ameeleza kuwa taasisi hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha kituo cha kulinda mifumo ya viwanda dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni pamoja na kituo cha taarifa za viwanda, ambavyo vinatarajiwa kuboresha usalama na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa sekta ya viwanda.
Mrindoko amesisitiza kuwa uwekezaji kwenye rasilimali watu hususan vijana wenye ujuzi wa kiteknolojia pamoja na upatikanaji wa rasilimali za kutosha, kutaiwezesha TIRDO kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi, kukuza uwekezaji na kuimarisha ushindani wa viwanda nchini.








